


Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Geita
WIZARA ya Nishati kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imejipanga kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanafikia kila kaya nchini Ili kufikia jitihada zake za kuimarisha afya za wananchi na kulinda mazingira nchini.
Hayo yameelezwa na Mhandisi Evance Kabingo wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika katika maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema, mikakati ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanatumia nishati isiyo na madhara kiafya wala kimazingira inatekelezeka kikamilifu.
Mhandisi Kabingo amesema kuwa matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni yamekuwa chanzo kikuu cha matatizo ya kiafya, hasa kwa akina mama na watoto, pamoja na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti hovyo.
“Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2030, angalau asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia kama vile gesi asilia (LPG), umeme, na majiko ya kisasa yanayotumia teknolojia rafiki kwa mazingira,” amesema Mhandisi Kabingo.
Ameongeza kuwa kampeni ya uhamasishaji inaendelea kufanyika kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa, wadau wa maendeleo, pamoja na sekta binafsi ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kutumia nishati safi na pia kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupikia kwa gharama nafuu.
Aidha amesema, REA imeweka mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya majiko banifu na gesi, ikiwa ni njia ya kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao huharibu mazingira na kuhatarisha afya.
“Tunatumia fursa hii ya maonyesho, ambapo hata wafanyakazi wa migodi wanahudhuria kwa wingi, kuwaelimisha kuhusu matumizi ya nishati safi kama gesi na majiko banifu. Hii ni kwa ajili ya kulinda mazingira na afya za watumiaji,” ameongeza.
Katika maonyesho hayo, wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa kwa kutembelea banda la REA, kununua majiko banifu na mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya wananchi 1,500 watakuwa wamepata huduma hiyo ifikapo mwisho wa maonyesho hayo.
Kwa mujibu wa REA, wananchi wanapewa majiko banifu na mitungi kwa utaratibu wa ruzuku ambapo jiko la gesi linatolewa kwa mchango wa asilimia 35 kutoka kwa mwananchi na asilimia 65 hufidiwa na Serikali huku majiko banifu, mwananchi huchangia shilingi 6,200 tu kati ya bei halisi ya shilingi 41,300, Serikali ikichangia asilimia 85 ya gharama.
Amewahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kupata elimu na vifaa hivyo, kama njia ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha matumizi ya nishati safi kwa maendeleo endelevu ya jamii.
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la REA wameipongeza Serikali kwa mpango huo wa kutoa ruzuku.
“Kabla ya mpango huu, wananchi wengi hatukuweza kumudu kununua majiko ya gesi. Lakini sasa, kwa shilingi 6,200 unaweza kupata jiko la kisasa, ni msaada mkubwa sana,” amesema Nasra Makungu, mkazi wa Ujamaa, Geita.
Naye Pelagia Paschal wa Nyaukumbu amesema kuwa bei ya kawaida ya majiko ilikuwa kikwazo kwa wananchi wa kipato cha chini.
“Kwa bei ya kawaida ya shilingi 50,000, wengi wetu hatuwezi kumudu. Lakini sasa kwa shilingi 6,200 kwa jiko banifu na shilingi 17,500 kwa mtungi mdogo, tumewezeshwa. Tunaishukuru sana Serikali,” amesema Paschal.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi