Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar
MAKUMBUSHO ya Taifa ya Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Japan, wamezindua rasmi maonesho maalum ya chakula cha jadi cha Kijapani Sushi, ikiwa ni sehemu ya kuelimisha jamii kuhusu urithi wa chakula kama sehemu ya utamaduni wa mataifa duniani.
Uzinduzi huo umefanyika Septemba 19, 2025, katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa jijini Dar-es-Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo raia wa Japan.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa,Dkt.Noel Lwoga, amesema onesho hilo linaonesha namna chakula kinavyoweza kutumika kama daraja la kuunganisha mataifa, kukuza utalii na kuhifadhi historia ya jamii.
“Sushi ni urithi wa dunia uliotambuliwa na UNESCO, wenye historia ya zaidi ya miaka 1,000. Kupitia onesho hili, tunajifunza namna ya kuenzi na kuonesha urithi wa chakula kama sehemu ya utambulisho wa Taifa,” amesema Dkt.Lwoga.
Amebainisha kuwa Tanzania pia ina hazina kubwa ya vyakula vya asili ambavyo vinaweza kutumika kutangaza utamaduni wa nchi na kuchochea utalii wa chakula, sawa na ilivyo kwa mataifa kama Japan.
“Chakula ni sehemu ya historia, ni utamaduni. Sasa tunaelekea kwenye upanuzi wa dhana ya utalii kutoka utalii wa wanyama pori hadi utalii wa chakula na tamaduni,hii ni fursa kwa Tanzania,”.
Aidha, amesema maonesho hayo yanalenga kuwavutia watalii wa ndani na nje, huku yakitoa fursa kwa Watanzania kuelewa na kuthamini tamaduni za mataifa mengine, sambamba na kujifunza njia bora za kutangaza vyakula vyao vya asili.
Dkt. Lwoga ametoa wito Watanzania kujitokeza kwa wingi kutembelea Makumbusho hayo katika kipindi chote cha maonesho, ambacho kitadumu kwa wiki mbili, ili kujifunza historia ya Sushi na kuonja ladha ya chakula hicho maarufu duniani.
“Maonesho haya ni daraja la diplomasia ya utamaduni kati ya Japan na Tanzania. Tunaamini chakula ni lugha ya urafiki na urithi wa chakula unachangia kuimarisha uhusiano wa mataifa,”amesema.

Kwa upande Naibu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Ueda Shoichi, amesema maonesho ya “Ninapenda Sushi” yameandaliwa kwa lengo la kutambulisha chakula cha jadi cha Kijapani Sushi, kwa Watanzania na wageni wa mataifa mbalimbali.
Shoichi amesema Japan inatumia maonesho hayo kama jukwaa la kuimarisha uelewa wa kiutamaduni kati ya mataifa hayo mawili.
“Tunaamini Tanzania ina nafasi kubwa kwa wapenda sushi. Hii ni fursa kwa watu kuja kuona na kujifunza kuhusu utamaduni wetu kupitia chakula,” amesema.
Shoichi ameongeza kuwa kwa sasa Tanzania haina mgahawa wa sushi, lakini matarajio ya baadaye ni kuwa na sehemu rasmi ya chakula hicho hapa nchini.
Aidha, alisisitiza kuwa Japan itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo utamaduni.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi