August 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Awamu ya pili ya uvutaji nyaya Chalinze–Dodoma kuanza kesho

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewakumbusha wananchi kuwa, kuanzia Agosti 11 hadi 17, 2026, mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovolti 400 Chalinze–Dodoma ataendelea na zoezi la uvutaji wa nyaya kwa awamu ya pili katika eneo la Kikombo na Mkonze, Dodoma, katika mradi huo ambao uko mbioni kukamilika.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Irene Gowelle, amesema hatua hiyo imekuja baada ya awamu ya kwanza ya uvutaji wa nyaya kutoka Chalinze hadi Mkambarani, Morogoro, kufanyika kwa mafanikio makubwa.

Amesema kutokana na kazi hiyo, baadhi ya mikoa itapata umeme kwa ratiba maalumu. Mikoa hiyo ni ile inayopatikana katika Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini Magharibi na Kanda ya Ziwa. Aidha, amesisitiza kuwa mikoa ambayo haitaathirika katika kanda hizo ni pamoja na Morogoro na Tanga.

Ameongeza kuwa mikoa inayotoka katika Kanda hizo zitakosa umeme kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni. Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kukamilisha mradi huo, ambao unatarajiwa kuwa na mchango chanya katika kuimarisha mfumo wa usafirishaji na upatikanaji wa umeme nchini.

‘’Hii ni awamu ya pili ya zoezi la uvutaji wa nyaya katika eneo la Kikombo na Mkonze Mkoani Dodoma, niwaondoe hofu wananchi kwamba tutaendelea kutoa ratiba za upatikanaji wa umeme kupitia mitandao yake ya kijamii, ili kuwawezesha wananchi kupanga shughuli zao kulingana na ratiba hiyo’’alisisitiza Bi. Gowelle.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026. Kukamilika kwake kutaongeza uwezo wa mfumo wa usafirishaji wa umeme nchini na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme yenye ubora na uhakika kwa wananchi.