
Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online ,Dodoma
MSEMAJI Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini kupitia uwekezaji na ufanisi wa Bohari ya Dawa (MSD).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Agosti 15,2025 Msigwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana kwa wakati katika vituo vya kutolea huduma za afya, jambo lililowezekana kupitia uwezeshaji mkubwa wa MSD katika maeneo yote manne ya msingi: uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya.
Kwa mujibu wa Msigwa, Serikali imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 642.1 katika kipindi cha miaka minne kununua bidhaa za afya kupitia MSD ambapokatika mwaka wa fedha 2024/25 pekee, MSD imepokea Shilingi bilioni 196.3 kati ya Shilingi bilioni 200 zilizotengwa, ikiwa ni utekelezaji wa asilimia 98 wa bajeti hiyo huku akisema katika kipindi hicho MSD imefanikiwa kuongeza vituo vya afya vinavyopokea huduma kutoka 7,095 hadi 8,776
Msigwa amwsema, lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote nchini kwa usawa na kwa wakati, sambamba na azma ya kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje kwa kuwekeza kwenye viwanda vya ndani na miundombinu ya uhifadhi na usambazaji.
Amesema ,Serikali imefanikiwa kutekeleza mipango hii kwa kuwezesha MSD kifedha, kuongeza maghala ya kisasa mikoani kama Dodoma na Mtwara, kuanzisha kampuni tanzu ya uzalishaji (MSD Medipharm), pamoja na kusambaza bidhaa za afya kwa wakati na kwa mizunguko ya kila baada ya miezi miwili badala ya mitatu.
Aidha amesema , bidhaa za afya za kinywa, mama na mtoto, pamoja na huduma za uchujaji damu zimeimarishwa, huku uwekezaji mkubwa ukielekezwa pia katika hospitali za kitaifa kama Muhimbili, MOI na JKCI.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utekelezaji wa sera ya viwanda pia umeimarika ambapo MSD imeanzisha viwanda vya uzalishaji wa barakoa na mipira ya mikono, na kuingia ubia na kampuni za kimataifa kama Rotabiogen ili kuzalisha dawa za sindano ndani ya nchi.
“Tunajivunia mafanikio haya ya kimkakati ambayo yameleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya nchini. Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa Watanzania,” amesisitiza Msigwa.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi