June 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya bilioni 40 kutatua kero ya maji Kasulu

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Kasulu

SERIKALI  imepeleka  zaidi ya  bilioni 40, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji safi na salama ili kutatua kero kwa  wananchi,kutokana na maeneo mengi ya Wilaya hiyo kuwa na malalamiko mara kwa mara juu ya ubora wa maji yanayopatikana.

Akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu Mjini (KUWSSA), Nuru Bagowe, ameipongeza serikali kwa kusikia kilio cha wananchi.

Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024 miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya zaidi ya  bilioni 40 imetekelezwa katika Wilaya hiyo na kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya maji safi.

Bagowe ametaja miradi hiyo kuwa ni wa Miji 28 ambao unagharimu kiasi cha bilioni 35,na utekelezaji wake umefikia asilimia 45, unatarajiwa kuhudumia wakazi wa kata 12 kati ya kata zote 15 zilizopo katika Halmashauri ya Mji Kasulu.

Mwingine ni ujenzi wa machujio ya mto Chai na Miseno unaogharimu kiasi cha milioni 385.5 ambao upo katika hatua za ukamilishaji na mradi wa maji Kidyama unaojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Enabel kwa gharama ya  bilioni 1.8.

Mradi mwingine  ni uboreshaji huduma ya maji katika mitaa ya Kabanga, Kimobwa, Mwilavya, Nyachijima, Nyarumanga, Kidyama na Kigondo unaogharimu bilioni 3.2.

Aidha katika kuhakikisha mfumo wa maji safi na maji taka unaboreshwa katika Wilaya hiyo, Bagowe, amesema wamepatiwa kiasi cha bilioni 2.2,kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa mfumo wa maji safi na maji taka.

Pia kiasi cha sh milioni 497.5 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu Mjini (KUWSSA),ambapo ujenzi wake  umefikia asilimia 70.