*Kupitisha magari takribani 20,000 kwa siku
*Gharama yake ingeweza kujenga zaidi ya kilomita 350 za barabara kiwango cha lami
*J.P.Magufuli kutumika kama alama na fahari ya taifa
Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Daraja la J.P Magufuli(Kigongo-Busisi),linatarajiwa kuzinduliwa Juni 19,2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhi Hassan,ambalo linaelezwa kupanua wigo wa fursa mbalimbali ikiwemo kuongeza idadi ya magari yanayovuka kati ya Kigongo-Busisi, kufikia wastani wa magari 20,000 kwa siku.
Hayo yamebainishwa Juni 8,2025, darajani hapo, Waziri wa Ujenzi,Abdallah Ulega wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mkoani Mwanza,kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali katika sekta ya ujenzi.

Ambapo amesema,kwa njia ya vivuko magari yaliokuwa yanapita ni wastani wa 600 -1,000, kwa siku,huku akisisitiza kuwa gharama iliotumika katika uwekezaji huo ni bilioni 716,ambazo zingeelekezwa kwenye barabara zingeweza kujenga zaidi ya kilomita 350 za lami.
Ulega,amesema daraja hilo litakuwa na uwezo wa kupitisha wastani wa magari matatu mpaka sita yasiozidi uzito wa tani 160, kwa wakati mmoja,pia lina urefu wa mita 17 kutoka kwenye maji mpaka juu ikiwa ni sawa na urefu wa zaidi ya ghorofa ya tano.Urefu huo ni mbali na nguzo zilizosimikwa ndani ya Ziwa Victoria.
Amesema daraja hilo lina faida lukuki ikiwemo, kuimarisha maisha ya Watanzania pamoja na kuthamini utu,kwani vivuko vilikuwa vinatumia muda mrefu hali iliyokuwa inachangia wananchi kuchelewa kufika eneo la kupatia huduma ikiwemo,wagonjwa na wajawazito.
“Kukamilika kwa daraja hili,kutakuwa faraja kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa ambao wamekuwa wakitumia saa mbili kuvuka upande mmoja kwenda mwingine,sasa muda wa kuvuka unatarajia kupungua na kufikia wastani wa dakika tatu.Pia linategemewa kuongeza shughuli za kiuchumi ndani na nje ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati,” amesema Ulega na Kuongeza:
“Daraja hili pia litakuwa moja ya alama na fahari ya taifa letu,ambalo Lina urefu wa Kilomita 3 na barabara unganishi zenye urefu wa Kilomita 1.66,hivyo kilifanya kuwa daraja refu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,”.
Huku akieleza kuwa vivuko vinavyotumika sasa katika eneo hilo la Kigongo-Busisi, vitapelekwa maeneo mengine nchini yenye uhitaji.

Hata hivyo Ulega,ameeleza kuwa,wakati Rais Samia,anaingia madarakani mwaka 2021, ujenzi wa daraja hilo ulikuwa umefikia takribani asilimia 25 huku Mkandarasi akiwa amelipwa fedha za awali takribani bilioni 130 hadi 150.
Kutokana na changamoto za kutetereka kwa uchumi wa Dunia baada ya janga la UViko-19, kulikuwa na wasiwasi kuwa kiasi cha bilioni 539.28,kitapatikana wapi kwa ajili ya kukamilisha mradi huo na ndoto za mtangulizi wake Hayati John Magufuli
“Fedha ambazo zimeingia hapa,ni nyingi na kazi hii imefanyika kipindi kigumu,watu tulikuwa tunasema hizi fedha za kukamilisha hili daraja itakuwaje,kwani zilitakiwa zaidi ya bilioni,”amesema Ulega.
Kwa upande wao wananchi wa Busisi wilayani Sengerema akiwemo,Fikiri Msimu,amesema daraja hilo litahudumia nchi takribani tatu ikiwemo Burundi,Rwanda na Uganda.
Hivyo ukiangalia idadi ya watu ya nchi hizo na magari yanayokwenda katika nchi hizo hivyo daraja hilo likifunguliwa litakuwa kichochezi cha uchumi na kuweza kuleta mabadiliko makubwa.
Tustawi Gamba,amesema,kufunguliwa kwa daraja hilo ni jambo jema kwa wananchi hususani wakazi wa Mwanza,Geita na maeneo mengine,watu watakuwa na njia rahisi na sahihi ya kusafirisha bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
‘Pia wasafiri watapata fursa ya kusafiri kwa wakati tofauti na awali ambapo tukifika hapa,tunakaa muda mrefu bila kupata huduma ya kuvuka,wakati mwingine kuanzia asubuhi mpaka saa sita mchana.Nashukuru Serikali imeliona hili na hatimaye imejaribu kulifanya kwa wakati,”amesema Xsavery.
Naye mmoja wa wafanyabiashara eneo la Busisi wilayani Sengerema,Moshi Idi,amesema,daraja litakapofunguliwa uendelezaji wa biasha yao utapungua kwa sababu gari hazitosimama katika eneo hilo na wateja wao wakuu ni abiria ambao utumia vivuko.
Hivyo ameiomba Serikali kuweka stendi katika eneo hilo ili watu watakaokuwa wanatumia njia hiyo kuweza kuwaunga mkono kwa.kununua bidhaa zao ikiwemo dagaa na samaki.



More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako