Na Irene Clemence
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam na taasisi ya Empower Limited wametangaza ushirikiano rasmi unaoendana na ajenda ya mabadiliko ya uchumi wa Tanzania kwa kufanya uwekezaji katika kuwapatia watu maarifa.
Ushirikiano huo utawezesha taasisi za elimu,makampuni ya kibiashara kushirikiana kupitia uratibu mzuri na utekelezaji wa mpango wa kutoa ujuzi unaotakiwa katika karne ya 21 ujulikanao kama Generation Empower (GenEm) katika shule zote za UDSM kwa kipindi cha miaka 5 ijayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa GenEm,Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Utafiti) Profesa Bernadeta Killian, amesema “Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinafurahi kushirikiana na Empower kuleta mabadiliko chanya yanayowezesha kuwapatia ujuzi wa karne ya 21 wanafunzi 250 kila mwaka sambamba na maarifa ya kusimamia vipaji vyao, kuchangamana na wateja wa makampuni ya kibiashara.
“Tunatoa wito kwa makampuni kuunga mkono programu hii ya Generation Empower-Wahitimu wake wa awamu ya kwanza watakuwa tayari kwa ajili ya kuingia katika soko la ajira ifikapo Juni mwaka wa 2021”,
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Empower Limited Miranda Naiman amesema “Kazi yetu kwa vijana wa Kitanzania katika kipindi cha miaka 11 iliyopita imehitimishwa na ushirikiano huu; tumefurahi kuleta pamoja wadau wote ili kujenga taifa letu kwa kuwekeza kwa viongozi wetu wa baadaye.
GenEm itafanya kazi sanjari na mipango ya kitaaluma ya UDSM kuwapa wanafunzi watakaofanikiwa kupitia katika programu hii ujuzi unaotakiwa kwa sasa, kuweza kupata maarifa zaidi ya taaluma zao na kuunganishwa katika fursa za ajira pindi wanapohitimu”.
Aliendelea kusema “Makampuni yanaweza kufaidika na wahitimu hawa wenye ujuzi mkubwa na vipaji ambao wanaweza kusaidia kusaidia kuongeza thamani katika shughuli zake kutokana na kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa wabunifu.
“GenEm inawezeshwa na Idara ya uwezeshaji Vijana kwa kushirikiana na kitengo cha Ubunifu na Ujasiriamali cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDIEC), ambacho kimejipanga kuhakikisha kinaongoza barani Afrika kwa kutoa mafunzo ya ujasiariamali na ubunifu.
Awamu ya kwanza ya mafunzo ya programu ya GenEm itajumuisha wanafunzi 250 kutoka fani tofauti za taaluma na yatachukua mwaka mzima ili kufanikisha mkakati wa kuwanoa walengwa kuhakikisha wanapata ujuzi unaotakiwa.
Mafunzo ya programu ya GenEm yataendeshwa kwa njia shirikishi na kwa vitendo zaidi ,watashiriki katika semina za kubadilishana mawazo, mafunzo kutoka kwa wataalamu, kupata mada kutoka kwa viongozi wa tasnia mbalimbali na mwisho washiriki kufanya miradi ya vikundi kuhusiana na mafunzo waliyopatiwa.
UDSM na Empower wanakaribisha wadau wote kushiriki katika GenEm ikiwemo sekta binafsi, watunga sera na washirika wahisani ili kufanikisha jitihada za kutoa kuendeleza ujuzi kupitia mpango wa ubia taasisi za umma na binafsi (PPP).
Programu hii ni ya kwanza kuanzishwa nchini na kuendeshwa kwa njia ya kipekee ambapo maudhui ya mafunzo yanayotolewa yanasimamiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha yanakidhi viwango vinavyotakiwa kwa kila tasnia na Empower inapoyatayarisha inahakikisha yanathibitishwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango