Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
UONGOZI wa klabu ya Yanga leo umemtangaza Zlatko Krmpotic kutoka Serbia (zamani Yugoslavia) kuwa kocha wao mpya anayeridhi mikoba ya Luc Eymael aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu kutokana na na kauli za kibaguzi alizozitoa kwa mashabiki na viongozi wa soka hapa nchini.
Yanga imeamua kumpa kandarasi ya miaka miwili kocha huyo kutokana na wasifu wake mzuri (CV) ambayo iliwafanya kuamini atawafikisha katika mafanikio wanayoyahitaji.
Awali klabu hiyo ilikuwa imeshamtambulisha kocha Cedric Kaze ambaye ameshindwa kujiunga na Yanga dakika za mwisho kutokana na matatizo ya kifamilia.
Jana katika mahojiano maalum na kituo cha redio cha Wasafi, Makamu Mwenyekiti wa Makati ya Mshindano ambaye pia ni Mkurugenzi wa uwekezaji wa GSM, Mhandishi Hersi Said amesema, baada ya Kaze kuwaweka wazi kile kitakachomchelewesha kutua Jangwali waliamua kurudi katika maombi yaliyotumwa na makocha mbalimbali na kuridhishwa na sifa za kocha huyo.
Amesema, kocha huyo ambaye aliwahi kuitumikia kwa mafanikio timu ya Taifa ya Yugoslavia kwa kuichezea mechi 400 pamoja na klabu mbalimbali alizowahi kuzitumikia pia ni miongoni mwa makocha bora ambao wameweza kuzipa mataji makubwa klabu mbalimbali.
Amesema kuwa ni imani yao kuwa, wasifu wake atautendea haki na kuwapa mafanikio makubwa ambayo aliyaonesha katika klabu nyingine alizopita.
Akiwa TP Mazembe, kocha huyo aliwawezesha kutwaa Kombe la Ubingwa la Klabu Bingwa Afrika na kufanya vizuri alipokuwa anazinoa timu za Zesco United, Polokwane City, APR na nyingine nyingi.
“Kumkosa Kaze haikumaanisha kuwa ndo mwisho wetu, tumefanikiwa kumchukua kocha huyo kutokea Polokwane na leo ataanza safari ya kuja nchini hivyo tunatarajia kumpokea kesho asubuhi”, amesema kiongozi huyo.
Kocha huyo atatu na kuungana na kocha wake msaidizi Juma Mwambusi ambaye naye anakandarasi ya mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo, kocha wa makipa kutoka Burundi Vladmir Niyonkuru, kocha wa viungo Riedoh Berdien, mchua misuli, Fareed Cassim, meneja Hafidh Saleh pamoja na mtunza vifaa.
“Tayari tulishamueleza kocha kuwa benchi letu la ufundi limekamilika na hakuwa na tatizo na hilo na ametueleza atafanya nao kazi hivyo hakuna sababu ya watu kuwa na wasiwasi, ” amesema Mhadhisi Hersi.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship