March 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wito umetolewa kwa viongozi wa dini kuliombea taifa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuiombea Tanzania, ili iendelee kuwa na amani na kuepuka athari za watu wanaotaka kuingiza nchi katika vurugu.

Pia amesema malezi na mafunzo wanayopata wanafunzi shuleni, hasa yanayosisitiza nidhamu na uwajibikaji ni msingi muhimu katika kujenga taifa imara lenye uzalendo.

Balozi Nchimbi amesema hayo wakati wa kikao cha umoja wa wanafunzi waliosoma shule ya sekondari Uru Seminari, kilichofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya ibada ya mazishi ya aliyewahi kuwa Baba Gombera wa shule hiyo, Padri Canute Shirima AJ.

“Nawaomba viongozi wa dini muendelee kuikabidhi nchi yetu kwa Mungu. Tuendelee kuiombea Tanzania, viongozi wake wa Serikali, CCM na hata wa upinzani, ili Mungu aendelee kutuongoza, kuna watu wenye nia ya kusababisha vurugu, hivyo ni muhimu sana tukaendelea kuilinda amani yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa malezi ya walimu yana mchango katika kujenga jamii yenye maadili na uzalendo, akisisitiza kuwa taifa linapaswa kuthamini juhudi za walimu katika kujenga kizazi chenye maadili.

“Hakuna aliyesoma Uru Seminari asiyetambua mchango wa kipekee wa Padri Shirima. Tulifundishwa nidhamu, uwajibikaji, bidii kazini, na umuhimu wa kufuatilia mambo kwa umakini. Mafundisho hayo yametufanya kuwa watumishi bora katika nyanja mbalimbali za maisha,” amesema Balozi Nchimbi.

Aidha, alitoa pongezi kwa umoja wa wanafunzi waliosoma Uru Seminari kwa mshikamano waliouonesha katika msiba wa Padri Canute, akiwahimiza kuendeleza umoja huo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.