March 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yavuna Shilingi Bilioni 3 ndani ya miezi nane

Na Mwandishiwetu, Timesmajira

MAKUSANYO ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Kagera yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/ 2025 ni Shilingi Bilioni 3.2Kagera ilipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 5.8 na mpaka mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu wa 2025 wamefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha kikiwa ni sawa na asilimia 82 ya lengo katika kipindi cha miezi nane.

Akizungumza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera, Nobert Mkopi amesema fedha hizo zimekusanywa kutokana na jitihada mbalimbali walizofanya katika usimamizi wa Sekta ya Madini katika halmashauri zote saba za Mkoa wa Kagera.

“Mkoa wa Kagera kwa maana Sekta ya Madini tunasimamia halmashauri zote saba kwa maana ya wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba, Biharamulo na Ngara, kuna shughuli mbalimbali za uchimbaji madini,”amesema Mkopi na kuongeza,

“Mkoa huu yanapatikana madini mbalimbali ikiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3), Madini ya Viwandani na Madini Ujenzi.“Maeneo ya Kyerwa yanachimbwa madini ya bati, yanachimbwa kihalali kwa leseni za uchimbaji mdogo lakini pia kuna leseni kubwa ya utafiti na madini haya yanachangia asilimia 32 mpaka sasa ya maduhuli tuliyokusanya ya Shilingi Bilioni 3.2 na fedha nyingine zinatoka kwenye madini mengine ikiwemo dhahabu na ada mbalimbali za vibali na leseni” amesema Mkopi

Aidha amesema mwenendo wa ukusanyaji maduhuli sio mbaya na hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wana imani watafikia lengo lililokusudiwa.

Katika hatua nyingine, Mkopi ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Kagera ambao una utajiri mkubwa wa madini mbalimbali ikiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3), Madini ya Viwandani na Madini ujenzi.