Na Mwandishi wetu,Timesmajira
KUELEKEA maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake , wahifadhi wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapaori Tanzania (TAWA) wametembelea Pori la Akiba Wamimbiki lililopo katika Mikoa ya Morogoro na Pwani kwa lengo la kuhamamisha utalii wa ndani.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, iliyofanyika Machi 1, 2025, Afisa Mhifadhi Mkuu, Zuwena Kikoti amesema wahifadhi wanawake wa TAWA wanaungana na wanawake wote nchini katika kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii duniani.
“Tumeungana na jitihada hizo kama wanawake kwa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kuvitangaza na kuwahamisha wanawake wa Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya jirani kutembelea hifadhi ya Wamimbiki katika kusheherekea siku ya wanawake duniani” ameongeza Kikoti.
Kwa upande wake, akimwakilisha Kamanda wa Pori la Akiba Wamimbiki Afisa Utalii, Gregory Kalokole amesema hifadhi ya Wamimbiki ni mpya na ya kimkakati yenye vivutio vingi vya utalii ikiwemo vivutio vya asili na vivutio vya utamaduni.

“Pori la Akiba Wamimbiki lina mandhari nzuri iliyozungukwa na miti ya miombo, wanyamapori kama vile Tembo, Simba, Viboko, Chui, Fisi, Tandala, Swala pala na Kulo na asilimia takribani 20 ya Mto Wami umepita ndani ya hifadhi” ameongeza Kalokole.
Sambamba na hilo, Kalokole alitoa shukrani zake kwa wahifadhi wanawake kutembelea hifadhi hiyo na alitoa rai kwa makundi mbalimbali ya wanawake na watanzania wote kwa ujumla kuja kutembela hifadhi hii.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yamepangwa kufanyika Kitaifa Jijini Arusha Machi 8,2025 na kauli mbiu ya mwaka huu ni Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.
More Stories
Prof. Kabudi atoa maagizo Saba Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari
Airpay yakabidhi Vishkwambi zitakavyotumiwa na ZEEA katika usajili, uombaji mikopo kidijitali
Tanzania yavunja rekodi,ongezeko la wanyamapori