November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani Wilayani Monduli akiongea na Watendaji mbalimbali wa Rea na Tanesco wakati wa ziara yake Wilayani Monduli jana .

Dkt.Kalemani aagiza Mkandarasi kusimamishwa kazi

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

WAZIRI wa Nishati Dk.Medard Kalemani amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya NIPO Group aliyekuwa akitekeleza mradi wa kusambaza Umeme Vijijini katika Jiji la Arusha kuachishwa kazi ya usambazaji umeme vijijini  kutokana na kazi anayofanya kusuasua.

Agizo hilo amelitoa jana wakati wa ziara yake Wilayani Monduli, Dkt. Kalemani amesema uwezo mdogo na usioridhisha wa Mkandarasi huyo katika kutekeleza kazi ya upelekaji umeme Vijijini ndio unaosababisha kuachishwa kazi.

Amesema Mkandarasi huyo amekuwa anafanya kazi isiyoridhisha na kukwamisha kasi ya ukuaji wa shughuli za kimaendeleo,kiuchumi na kijamii ambazo zingefanyika kwa haraka  na wananchi kupata nishati ya umeme.

“Bila kukiuka utaratibu wowote, mfuteni kazi Mkandarasi huyu na apewe mwenye uwezo vinginevyo Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini(REA) mfanye kazi hii wenyewe ili kuhakikisha wananchi wapate  umeme Mwezi ujao”, amesema Dkt Kalemani.

Aidha amesema Mkandarasi huyo alipewa kazi ya kusambaza umeme katika vijiji 126 vya Mkoa wa Arusha na hadi mkataba wake unakwisha alikuwa ameunganisha vijiji 59 pekee. 

Mkurugenzi Mtendaji wa REA, Mhandisi Amos Maganga ameeleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo katika Mikoa mingine anayofanya kazi ikiwemo Mwanza na tayari wameanza taratibu za kumfutia kazi hiyo kwa Mkoa huo pia.