January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Homera:Viongozi  hamasisheni  ununuzi wa hatifungani ya miundombinu ya Samia


Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia Mkoa, Wilaya, Vijiji hadi Mitaa,kuhamasisha wananchi, wafanyabiashara, na wadau wengine kununua hatifungani ya miundombinu ya Samia (Samia Infrastructure Bond).

Huku akisisitiza kuwa kununua hatifungani hiyo kutasaidia kufikia malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya barabara nchini.

Akifungua mafunzo ya mauzo ya hatifungani hiyo yaliyofanyika Desemba 19,2024,mkoani Mbeya, Homera amesema kuwa programu ya Samia Infrastructure Bond ni muhimu kwa utekelezaji wa miradi ya barabara za kisasa, hasa katika Mkoa wa Mbeya, ambapo miundombinu mingi inakabiliwa na changamoto kubwa.

“Miundombinu mingi ya Mkoa wa Mbeya ni changamoto, lakini juhudi zinaendelea,uchumi ni barabara, na tunahitaji barabara za kisasa kujengwa. Hata hivyo, tunajenga barabara za njia nne kwa mapato ya ndani, na miradi ya maji ya chanzo cha Mto Kiwira,inatekelezwa kwa mapato haya haya ya ndani,” amesema Homera. 

Homera amesema kwamba Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA)benki ya CRDB ,Tamisemi wanaenda kuweka historia ya kuondoa changamoto ya miundombinu nchini kupitia programu hiyo na kikubwa ni kuwekeza na kuweka fedha ili kuendeleza uchumi binafsi na Tanzania kwa ujumla.

Hata hivyo Homera amesema kuwa kupitia programu hiyo ni vema kuungana kwa pamoja na kuhimiza ununuzi wa bond ili kuweza kutatua changamoto za barabara za Isyesye na maeneo mengine ya Mkoa Mbeya.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA  Ileje, Lugano Mwambingu,amesema kuwa barabara zinazojengwa na TARURA mara nyingi zina uzito mdogo, na wananchi wanapozitumia vibaya kwa kupitisha mizigo mikubwa, barabara hizo huharibika mapema.

 Amesisitiza kuwa, kupitia programu ya Samia Infrastructure Bond, TARURA itapata fedha za kutosha ambazo zitasaidia kuboresha miundombinu ya barabara kwa kujenga barabara zinazoweza kubeba uzito mkubwa.

Jenipher Tondi ni Meneja Kanda Nyanda za juu kusini Benki ya CRDB amesema kuwa kupitia programu hiyo TARURA itanufaika kwa kiwango kikubwa na kuweza kutekeleza miradi kwasababu haitakuwa na utegemezi wa fedha za  Serikali tu.Huku fedha ambazo zitakusanywa zitaenda kusaidia kwenye miundombinu chini ya TARURA.