November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFS yatakiwa kuwa na utambulisho unaofanana

Na Tulizo Kilaga, Dodoma

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Allan Kijazi, amelitaka Jeshi la Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha inakuwa na jina moja litakaloitambulisha asali inayoizalisha nchini.

Ameyasema hayo leo alipotembelea banda la TFS katika maonesho ya 28 ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) Kanda ya Kati 2020 yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni nje kidogo ya Mji wa Dodoma.

Dkt. Kijazi anasema hana shaka na kazi kubwa inayofanya na TFS katika kuzalisha asali lakini anashangazwa kuona mabanda yake tofauti yakionyesha asali zenye utambulisho tofauti.

“Nimeona asali toka Sao Hill na hapa naona Asali Halisi ya TFS hii inakuwaje? Hizi zote si asali zenu kwanini ziwe na utambulisho tofauti? labda kama kuna ajenda iliyojificha lakini nyote nyinyi ni wamoja hamna sababu ya kujitambulisha tofauti sokoni,”

“Lakini pia ni vema katika maonesho haya pamoja na mambo mengine mngekuwa na banda moja tu la Asali ya TFS ambalo ndani yake mnegekuwa na bidhaa zote zinazozalishwa na nyuki kutoka maeno yenu mbalimbali,” amesema Dkt. Kijazi.

Hata hivyo, Dkt. Kijazi alisema licha ya kuona asali hizo kwenye maonesho hayo, hajawahi kuziona kwenye maeneo mbalimbali ya Kaskazini na kuitaka TFS kuongeza uzalishaji pamoja na usambazaji.

“Sasa nchi yetu imeingia katika uchumi wa kati ni muda muafaka kwenu kuendelea kupiga juhudi zaidi ya pale mlivyokuwa mnafanya katika uzalishaji na usambazaji wa asali ili muendelee kupaa kuliko hivi ambavyo mmefikia sasa” amesema Dkt.Kijazi.

Kwa upande wake Kassim Ally, Afisa Uenezi wa Jeshi la Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania alisema tayari TFS imeshakamilisha taratibu zote za usajili wa jina litakalokwenda kuitambulisha asali ya wanayozalisha na sasa itatambulika kwa jina moja, Misitu Honey.

Ally anasema kwa upande wa uzalishaji asali TFS umeanzisha hifadhi mpya 8 za nyuki kutoka idadi ya misitu 6 mwaka 2015 hadi kufikia hifadhi 14 mwaka 2019.

Alizitaka hifadhi hizo kuwa ni Kanda ya Kati (Manganze-Mzaree, Songolo, Lebba-Jumbe, Mialo-Kwamtoro, Aghodi na Msemembo), Kanda ya Magharibi (Buha –Kibondo), Kanda ya Kaskazini (Kangala, Kwenyunga Magiri, Kwamba na Muheza) na Kanda ya Nyanda za juu Kusini (Kipambawe, Shinji, Malinga, Chilangu).

Aliongeza kuwa kuongezeka kwa manzuki zinazosimamiwa na TFS kutoka 72 mwaka 2015 hadi 256 yenye mizinga 12,936 mwaka 2019 ambayo imetundikwa katika maeneo ya misitu mbalimbali nchini kumeongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki hasa asali na nta kutoka tani 4 mwaka 2015 hadi 30 mawaka 2019.