September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kawaida awasihi viongozi wa UVCCM kujifunza namna ya kuishi kwenye misingi ya uongozi

Na Mwandishi wetu,Iringa

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Mohammed Ali Kawaida , amewasihi Viongozi wa UVCCM Mikoa na Wilaya zote nchini, kujifunza namna ya kuishi kwenye misingi ya uongozi kwa vitendo huku wakizingatia Katiba, Kanuni na Miongozo ya Chama Cha Mapinduzi.

Pia amewataka viongozi hao, kuhamasisha ushiriki wa vijana kikamilifu katika uandikishaji katika Daftari la kudumu la wapiga kura linazotazamiwa kufungiliwa rasmi Julai 20, 2024 Mkoani Kigoma.

Kawaida ameyasema hayo alipokua anahutubia Viongozi na Watendaji hao katika Ufungaji wa mafunzo ya Viongozi na Watendaji wa UVCCM Mikoa na Wilaya zote nchi nzima yaliyofanyika Chuo chua Ihemi Mkoani Iringa kuanzia Julai11 hadi 17,2024.

Amesema mafunzo hayo waliyoyapata yanastahili hivyo yataenda kurahisisha utendaji kazi wao katika maeneo yao ya kazi.

” Niwasihi sana nendeni mkaishi katika misingi ya Uongozi kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na Miongozo ya Chama chetu,”amesema na kuongeza

“Nimefurahishwa sana namna ambavyo mmekua wasikivu, mmeishi kwa ushirikiano, mmeishi kwa umoja na kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kipindi chote cha mafunzo yenu, mmedhihirisha kuwa ninyi ni Viongozi wa kweli na mmekua katika misingi ya uongozi ndani ya CCM,”amesema Mwenyekiti Kawaida.

Aidha amewasisitiza kudumisha ushirikiano wa viongozi wa umoja wa Vijana wa CCM na Viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu katika maeneo yao.

“Ndugu viongozi niwasihi sana twendeni tukafanye kazi kwa ushirikiano sisi kwa sisi na tupendane mpaka watu waliopo nje washangae, lakini pia tushirikiane na viongozi wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yetu kwenye maeneo yetu,”amesema.

Kawaida amesema ni vema viongozi hao wakafatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama na kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika maeneo yao.

Akizungumzia Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Amesema viongozi lazima wawe mstari wa mbele katika kuhamasisha vijana waweze kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

“Sisi viongozi lazima tuwe mstari wa mbele katika Uhamasishaji wa Vijana kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, twendeni tukawape hamasa ya kutosha vijana kujiandikisha kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika chaguzi zote”,amesema.

Mafunzo hayo yamefungwa na Mwenyekiti Kawaida,Ihemi Mkoani Iringa ambapo awali yalifunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi Julai 11,2024