September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania mwenyeji Jukwaa la ununuzi wa umma Afrika Mashariki

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

TANZANIA imepata fursa ya kuandaa na kuratibu Jukwaa la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki litakalifanyika kuanzia Septemba 9 hadi 12 mwaka huu mkoani Arusha.

Ambapo nchi za Afrika Mashariki zitashiriki kama Kenya,Uganda,Burundi,Rwanda,Sudani ya Kusini,Somali na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo huku Tanzania ikiwa mwenyeji wake.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Julai 18,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa Umma (PPRA) Eliakim Maswi ambapo amesema ufunguzi wa jukwaa hilo unatarajiwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye kupitia hafla hiyo pia atazindua Mfumo wa Ununuzi wa Kielektroniki(NeST).

Amesema kuwa jukwaa hilo linatarajiwa kukusanya washiriki wapatao 1000 kutoka katika nchi za Afrika Mashariki kwaajili yakujadili ajenda ya ununuzi wa umma katika eneo hilo.

“Washiriki hao watatoka katika sekta ya umma, sekta binafsi, mashirika ya kitaaluma,asasi za kiraia na taasisi za mafunzo na nyinginezo,”amesema.

Pamoja na hayo Maswi ametaja baadhi ya faida zinazopatikana kupitia jukwaa hilo kuwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na ubadilishaji wa maarifa kati ya vyombo vya udhibiti wa ununuzi kutoka nchi wanachama wa Afrika Mashariki.

Vilevile kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utendaji kazi wa serikali kwa kuboresha mifumo ya kitaasisi na kuwajengea uwezo wafanyakazi  wa ununuzi ili kutekeleza majukumu na kazi zao kwa ufanisi kwa kuzingatia kanuni na viwango bora.

Lakini pia jukwaa linaipa PPRA  na wadau wengine  fursa ya kupata ujuzi na upasuaji habari ambao ni muhimu Kwa ajili ya kuendeleza uwazi na thamani ya fedha katika mikataba ya umma.

Hata hivyo amesema tangu ulipoanza kutumika mfumo wa NeST julai 2023 mfumo huo umewezesha kupunguza muda wa michakato ya ununuzi wa umma,kupunguza gharama za michakato, kuziba mianya ya rushwa ,kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na usalama wa taifa za watumiaji.