September 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtuhumiwa wa madawa ya kulevya ashikiliwa Dar

Na Bakari Lulela, TimesMajira Online

MAMLAKA ya kudhibiti na kupambana na madawa za kulevya inamshikilia Shabani Musa Adam (54) mkazi wa jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kutengeneza dawa za kulevya na kuyauza sehemu mbalimbali.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa nyumbani kwake Juni 11 mwaka huu manzese kilimani akitengeneza dawa aina ya heroin kwa kutumika dawa tiba zenye asili ya kulevya akichanganya na kemiikali bashirifu.

Akizungumza jijini Dar es salaam Kamishna jenerali wa MAMLAKA ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Aretas James Lyimo alisema mara nyingi anapozitengeneza dawa hizo huzisafirisha kwa kutumika mabasi ya abiria kama abiria kuelekea mikoa mbalimbali nchini.

“MAMLAKA ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya imekamilisha kanzi data (data base) ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya na imeanza uchunguzi juu ya watu hao, wengi wamebainika wapo ndani ya nchi na wengine nje ya nchi,” alisema Lyimo

Aidha  Lyimo alisema kuwa kati ya hao Wana biashara nyingine halali lakini wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kufanya utakatishaji sehemu mbalimbali.

Hata hivyo mtuhumiwa huyo ameeleza MAMLAKA hiyo kuwa siku za nyuma alikuwa akitengeneza dawa hizo za kulevya katika nchi za bara la Asia kwenye magenge ya wazalishaji waadawa ya kulevya na pia alikuwa akitumika kama mbebaji.

MAMLAKA inatoa wito kwao kuachana mara moja na biashara hiyo na kujikita kwenye biashara halali kwani uchunguzi dhidi yao unaendelea.

Katika nyakati nyingine MAMLAKA hiyo inamshikilia mtu moja aliyetambulika kwa jina la Mbaba Rabbini ISSA mtanzania mwenye pasipoti namba TAE442718 ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Melchior Ndadaye Bujumbura Burundi akiwa na kiasi cha kilogramu 3.8 za skanka ambapo dawa hizo zilikuwa zimefichwa kwa kushonewa ndani ya begi.

Vilevile kupitia ofisi za Kanda za MAMLAKA zimefanya operasheni katika mikoa ya mwanza, Dodoma, Mtwara na Mbeya na kukamata gunia 285 za bangi kavu, kilogramu 350 za aina mbalimbali ya dawa za kulevya, milimita 115 za dawa tiba zenye asili ya kulevya pamoja na lita 16,523 za kemiikali bashirifu.

MAMLAKA hiyo imewatunuku nishani baadhi ya watu  na taasisi walioshiriki kupambana na madawa ya kulevya kati ya hao alikuwepo profesa Janabi kutoka katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mkurugenzi wa kituo cha ITv na radio one  Joyce Muhavile.