Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
NAIBU Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora (Kitete) na kukutana na watumishi ili kupokea taarifa na kusikiliza kero zao.
Katika mkutano huo baadhi ya Watumishi wameeleza kukabiliwa na matatizo mengi ambayo hayajashughulikiwa na Menejimenti kwa muda mrefu licha ya Hospitali hiyo kuingiza mapato kila mwezi, na kueleza kuwa hili linawavunja moyo.
Wametaja baadhi ya kero hizo kuwa ni kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu ikiwemo fedha za likizo, matibabu, kutopandishwa vyeo na marupurupu mengine ya kiutendaji.
Aidha wamelalamikia hali ya mazingira ya hospitali hiyo kutoridhisha hususani katika wodi ya wazazi na maeneo mengine licha ya kuwepo Kampuni iliyopewa kandarasi ya kufanya usafi katika hospitali hiyo.
Baadhi ya watumishi wamemweleza Naibu Waziri kuwa Kampuni hiyo haina uwezo wa kazi waliyopewa na kudai kuwa wahusika wanakumbatiwa na Uongozi, kwani licha ya kulalamikiwa hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.
Awali Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Mark Waziri amemweleza Naibu Waziri kuwa Hospitali hiyo inaendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa huduma za afya kwa jamii kwa weledi mkubwa licha ya changamoto kadhaa zilizopo.
Amebainisha baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kutolipwa baadhi ya stahiki za watumishi ikiwemo posho, likizo, matibabu na malimbikizo mengine, huku akitaja sababu kuwa ni kupungua kwa fedha za OC walizokuwa wanaletewa.
Mhasibu wa Hospitali hiyo Samwel Mgula amekiri stahiki nyingi za Watumishi kutolipwa tangu mwezi Januari hadi sasa kutokana na ukosefu wa fedha kwani OC wanazoletewa kila mwezi hazitoshelezi.
Akitoa maelekezo ya Serikali, Naibu Waziri Dkt Mollel amesema kuwa sh mil 267 zinazoletwa na serikali hazitumiki vizuri, zinaingia mifukoni mwa baadhi ya Viongozi wa Hospitali, hili halikubaliki hata kidogo.
‘Kama mnapata zaidi ya sh mil 267 kila mwezi mnashindwaje kuwalipa stahiki zao na mbaya zaidi wengi wao wana madai ya muda mrefu, na hela zinaletwa kila mwezi, katika hili Menejimenti mmeshindwa kazi, tutafanya maamuzi’, amesema.
Dkt Mollel ameongeza kuwa kabla hajafika hospitalini hapo aliambiwa kuwa hospitali inanuka, alithibitisha kuwa ni kweli kwani ameingia katika moja ya wodi ya wazazi na kukuta hali ya usafi sio nzuri.
Amebainisha kuwa kama watumishi wana malalamiko mengi na usafi hauridhishi, hii ni ishara ya Menejimenti kufeli, hivyo akaahidi kuwa watachukua hatua stahiki kwa watumishi wote wasiowajibika ipasavyo ili kuboresha utoaji huduma.
Ameelekeza Timu ya Afya ya Mkoa (RHMT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kusimamia utendaji wa hospitali hiyo wakati Wizara ikilifanyia kazi suala hilo, aliahidi kurudi ndani ya wiki 2 ili kutoa uamuzi wa Wizara.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Deusdedit Katwale amempongeza Naibu Waziri kwa dhamira yake njema ya kuboresha utendaji wa hospitali hiyo.
Ameahidi kuwa kama Mkoa wataendelea kusimamia weledi katika suala zima la utoaji huduma za afya katika hospitali hiyo ya Mkoa huku akiahidi kuwa wiki mbili alizowapa watazitumia kufanya marekebisho ya kiutendaji.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa