December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mvutano vyama vya wafanyakazi kikwazo vikao baraza la wafanyakazi Wizara ya ardhi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Vikao vya baraza la Wafanyakazi vya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeelo ya Makazi havikufanyika kwa wakati kama ilivypongwa kufuatia watumishi wa Wizara hiyo kuwa wanachama wa vyama viwili vya wafanyakazi ambavyo ni TUGHE na TALGWU vyama ambavyo vimekuwa na mvutano juu ya uendeshaji vikao hivyo.

Akiongea mjini Morogoro leo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Lucy Kabyemera ambaye alimwakilisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa alisema sintofahamu iliyopo haileti afya njema kwa maendeleo ya watumishi wa Wizara yake.

‘’Kwa mujibu wa mkataba ni kwamba vikao vinapaswa kufanyika mara mbili kwa mwaka kwa masikitiko makubwa Wizara yetu imeshindwa kufanya vikao hivyo kwa wakati kutokana na changamoto iliyojitokeza ambayo ni uwepo wa Vyama vya Wafanyakazi viwili ndani ya Wizara yetu’’.Aliongeza Lucy Kabyemera Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.’’

Naibu Katibu Mkuu Kabyemera aliongeza kuwa hali ya kuwa na Chama zaidi ya kimoja ndani ya Wizara ilitokana na uamuzi wa Serikali wa kuwahamisha watumishi wa Sekta ya Ardhi kutoka Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuwaleta Wizara ya Ardhi Mwaka 2019.

Bi. Lucy Kabyemera aliongeza kuwa uamuzi huu ulipelekea Wizara kuwa na makundi mawili ya wanachama wa vyama vya wafanyakazi wanaotokana na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), ambacho kina wanachama 295 na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) chenye wanachama 792.

Aidha kutokana na uwepo wa vyama hivyo, Wizara ilikusudia kuunda baraza jumuishi la wafanyakazi ili kuwa na wawakilishi wa vyama hivyo viwili. Hata hivyo, Baraza hili limelazimika kufanyika kwa kibali cha nyongeza kwakuwa bado vyama hivyo havijafikia maridhiano ya kuwa na Baraza shirikishi.

‘’Nawasihi vyama kurejea katika meza ya majadiliano na kuchochea utendaji kazi wa Wizara ya Ardhi kwakuwa vyama vyote ni sehemu muhimu ya Wizara hii. Aidha, nimuombe Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi pamoja na Kamishna wa Kazi kusaidia katika kumaliza sintofahamu ya uhalali wa Vyama hivi ndani ya Wizara ya Ardhi, kwakuwa ninaamini vyama vyote vina lengo sawa la kusimamia haki na ustawi wa Wafanyakazi.’’Alinukuliwa akisema Bi. Lucy Kabyemera Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo kwa niaba ya Waziri Silaa amewakumbusha wajumbe wa Baraza hilo kuhusu vipaumbele vyake tangu alipoingia katika Wizara yake aikibainisha kuwa moja ya vipaumbele ni utatuzi wa migogoro ya ardhi ambapo nilitoa siku 100 kwa kila mtendaji kutatua mgogoro kwenye ngazi yake ya utendaji.

Aidha, Waziri alitoa maelekezo kuhusu usimamizi wa maeneo ya wazi na maeneo ya huduma ikiwemo kuhimiza matumizi sahihi ya ardhi na ubadilishaji holela wa matumizi ya ardhi mfano ujenzi wa vituo vya mafuta, kukamilishwa zoezi la urasimishaji na kuboresha utendaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya

Mengineyo ni maendeleo ya makazi na upimaji ardhi na utendaji kazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuwataka wote wanaoguswa na vipaumbele hivi kufanya kazi kwa bidii ili nitakapofanya tathmini ya kila eneo, asiwepo atakayeathirika.

Baraza hili linakutana kujadili kwa kina Makadirio ya Mipango na Matumizi kwa mwaka 2024/2025 na kuweka mipango ambayo inatekelezeka itakayosaidia kuleta maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi.