November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Siasa Nyamagana,yawaka kusuasua ujenzi wa barabara Buhongwa-Igoma

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Wilaya ya Nyamagana imeishukia kampuni ya ukandarasi ya ZHONGMEI Engineering Group ya China, inayojenga kwa kiwango cha lami barabara ya Buhongwa hadi Igoma yenye urefu wa km 14 ikimtaka kuukamilisha mradi huo kwa mujibu wa mkataba.

Imesema, mradi huo wa uboreshaji wa Majiji na Miji (TACTIC),unaojengwa kwa gharama ya zaidi ya bilioni 22.7 bila VAT, umefikia asilimia 4.6 kati ya asilimia 7.6,hivyo uko nyuma kwa asilimia 3 tofauti na mpango kazi uliowasilishwa na kuidhinishwa,tangu kusainiwa kwa mkataba Septemba 2023.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Nyamagana,Mwenyekiti wa CCM wilayani humo,Peter Bega amesema,mradi wa barabara ya Igoma hadi Buhogwa ni kilio cha kiuchumi cha wananchi wa Jiji kwa ujumla ambapo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alitoa fedha za kuutekeleza,ili kusiwe na changamoto mkandarasi asimamiwe ukamilike kwa wakati.

“Mradi huu ni kilio cha Nyamagana kwa miaka mingi, ni ahadi iliyotolewa na serikali ya awamu ya nne.Rais Dk.Samia ametoa zaidi ya sh. bilioni 22 na mkandarasi ameshalipwa sh. bilioni 3.409, hatuoni kwa nini mradi unasuasua,tuusimamie na hatutaki excuse (samahani),”amesema.

Bega amewatoa wananchi hofu ya kukosa barabara kuwa itakamilika kwa sababu Rais Samia alishatoa fedha,kazi ya kusimamia si yake bali ya aliowapa dhamana ili kazi ifanyike kwa wakati na kuleta manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema mradi huo ukikamilika utafungua uchumi wa wananchi wa Nyamagana,ni mtaji wa kisiasa wa CCM na kuonya wanaotaka kuukwamisha wanaikwamisha Serikali na Chama Cha Mapinduzi,usipokamilika na kuusemea,uchaguzi ukifika wapinzani wataunyooshea vidole na kutupunguzia kura.

Mwenyekiti huyo wa CCM Nyamagana amesema haiwezekani kukosa ushindi (kura) sababu ya mtu mmoja kutotimiza wajibu na hakuna sababu ya kumsikiliza mkandarasi,lazima asimamiwe mradi ukamilike kwa wakati.

“Fedha zipo, tunakwama wapi? ni fedheha msimamizi na mshauri wa mradi kutofautiana lugha.Mradi huu ni ahadi ya serikali ya awamu ya nne pia awamu ya tano,Rais Samia ana imani na ninyi, alishasema ataitekeleza miradi yote kwa wakati,kwa nini tufike 2025,ajira zipatikane kwa vijana mradi ulikopita,”amesema Bega.

Mhandisi wa barabara wa kampuni ya ZHONGMEI Engineering Group,Wang Zhengkai,amesema changamoto ni gharama kubwa zilizowasilishwa na MWAUWASA na TANESCO za kuhamisha miundombinu ya maji na umeme.

Ambapo MWAUWASA iliwasilisha sh.milioni 800 na TANESCO zaidi ya sh.bilioni Moja ili hali fedha zilizotengwa na mradi ni sh. milioni 250 za umeme,maji na simu.

Naye mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo ya Siasa,Dkt.Kerebe Luteri amesema aliopewa dhamana kwa niaba ya wananchi,wasimamia barabara hiyo ijengwe na kukamilika kwa wakati,haoni hoja ya msingi mradi kuchelewa sababu ya miundombinu ya maji na umeme wakati usanifu na upembuzi yakinifu ulifanyika.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi kwa niaba ya watendaji wa serikali amesema wamepokea maelekezo ya kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi huku akionya wanaotaka kukwamisha mradi huo wa barabara kufanya ubadhirifu na kuiba vifaa wakatafute kazi nyingine.

Awali Mhandisi Jane Mdulla kwa niaba ya Mratibu wa Mradi huo wa TACTIC,Mhandisi Dustan Kishaka,amesema unalenga kujenga uwezo wa mamlaka za serikli za mitaa kujiendesha zenyewe kupitia mapato ya ndani baada ya kuboresha miundombinu wezeshi ya kuvifikia vyanzo mbalimbali vya mapato na utainua uchumi wa Jiji la Mwanza.

Pia,amesema mbali na changamoto ya gharama za kuhamisha miundombinu kuwa juu,nyingine ni mkandarasi kutoleta magari na mitambo kwa mujibu wa mkataba amewasilisha asilimia 52.5 na kusababisha kazi kutofanyika kwa kasi ambapo alishaonywa mara tatu kwa barua.