November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nderiananga aongoza dua ya kumwombea Rais Samia

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameongoza dua ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pia ameungana na Viongozi wa Dini na wananchi kupata Iftar ya pamoja.

Akizungumza mara baada ya dua hiyo iliyofanyika jana Aprili 7, 2024 katika Kituo cha kulea watoto yatima cha Rahmaan kilichopo Chang’ombe Jijini Dodoma, Mhe. Nderiananga amesema kuwa uamuzi huo wa kufanya dua ya kumuombea Rais Samia ni kwa sababu ya mambo mengi aliyoyafanya katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, maji, afya na miundombinu.

Aidha, Mhe. Nderiananga amewasihi Watanzania kuendelea kudumisha amani na utulivu ili Taifa liendelee kuwa katika hali ya amani na usalama.

“Tumeamua kufanya dua hii maalum ya kumuombea Mhe. Rais na viongozi wetu wa Serikali pamoja na wazazi wangu”. Amesema Mhe. Nderiananga.

Ameongeza “Tunashukuru sana uongozi wa kituo hiki kwa dua nzuri kwa watoto na malezi mazuri ya hawa watoto wetu naamini wamejisikia vizuri na kufurahi tulivyowatembelea leo”.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewashauri watoto hao wasome kwa bidii ili kutimiza ndoto zao huku akiwataka kuepuka kujiingiza katika makundi mabaya yatakayosababisha kutotimiza malengo yao.

Mkurugenzi wa Kituo hicho Bi. Rukia Hamis Abdallah ameeleza kwamba kituo hicho kinachohudumia watoto 120 kilianzishwa kwa lengo la kujiendeleza kielimu katika maadili mema ya dini, kusaidia watoto pamoja na watu wanaoishi katika mazingira magumu.