Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bumbuli iliyopo wilayani Lushoto mkoani Tanga imeendelea kutoa motisha kwa walimu wa shule za sekondari kwa kununua A na B zitakazopatikana kwenye shule zao kutokana na wanafunzi wao kufanya vizuri.
Zawadi hizo zitawafikia pia wadau wa elimu wakiwemo Maofisa Elimu Kata (WEO) na Watendaji wa Kata ambao shule zilizopo kwenye maeneo yao zikifanya vizuri.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bumbuli Baraka Zikatimu kwenye hafla ya kukabidhi zawadi ya fedha kwa walimu, shule, maofisa elimu kata, watendaji wa kata na mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza (division one) ya alama saba (point 7).
Ambapo Prisca Seleman Ally (16) ambaye ni mwanafunzi alitepatiwa kiasi cha 500,000 na Halmashauri hiyo baada ya kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2023 akitokea shule ya sekondari Kizimba ambayo ni shule ya kata iliyopo Kijiji cha Galambo, Kata ya Bumbuli.
Zikatimu amesema Mkuu wa Shule atakaewezesha wanafunzi kupata A kwenye mitihani ya kitaifa, kuanzia A ya kwanza hadi ya nne, watainunua kwa sh. 10,000,kuanzia A ya tano na kuendelea, watainunua kwa sh. 12,000 huku Mkuu wa Shule atakawezesha kupata B kuanzia ya kwanza hadi ya 20 watainunua kwa sh. 5,000,B ya 21 hadi 40, itanunuliwa kwa sh. 7,000, na B ya 41 na kuendelea itanunuliwa kwa sh. 10,000.
“Shule itakayopata daraja la kwanza hadi la nne (div. 1-4), yaani kutokuwa na zero (sifuri), itapata sh. 500,000,itakayopata daraja la kwanza hadi la tatu (div. 1-3) itapata sh. milioni moja,itakayopata daraja la kwanza na pili (div. 1-2) kupata sh. milioni mbili, na shule itakayokuwa na daraja la kwanza tu (div.1) itapata sh. milioni tatu,”ameeleza Zikatimu na kuongeza
“Halmashauri tunafanya haya ili kutoa motisha kwa walimu, shule na wadau wengine wa elimu kama maofisa elimu kata na watendaji wa kata, tunataka Halmashauri ya Bumbuli ifanye vizuri kitaaluma kitaifa,”.
Katika hafla hiyo, Halmashauri ya Bumbuli ilikabidhi kiasi cha sh. milioni 13.85 fedha taslimu kama zawadi kwa wakuu wa shule, walimu wa taaluma, shule, maofisa elimu kata na watendaji wa kata waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa mwaka 2023 ambazo zimekabidhiwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ameir Sheiza.
Awali, Ofisa Elimu Taaluma Sekondari Halmashauri ya Wilaya Bumbuli Simon Shelukindo amesema hali ya ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne (CSEE) kwa kipindi cha miaka mitatu imekuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka kwenye halmashauri hiyo.
“Matokeo ya mwaka 2023 yakilinganishwa na matokeo ya 2022, kuna ongezeko la asilimia 0.58,2022 Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli ilikuwa ya tatu kati ya halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga, wakati mwaka 2023, Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli ilikuwa ya nne kati ya halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga,” amesema Shelukindo.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunziÂ
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu