Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Kahama.
WACHIMBAJI wadogo wa madini ya dhahabu wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuunda timu za uokozi ambazo zitafanya kazi ya uokoaji haraka pindi panapotokea janga lolote kwenye maeneo ya migodi ikiwemo kuporomoka kwa duara au mchimbaji kuteleza na kuangukia ndani ya duara.
Ushauri huo umetolewa na Meneja Mradi kutoka Shirika la Solidaridad, Mhandisi Winfrida Kanwa kwenye mafunzo ya wakaguzi na mameneja wa migodi midogo ya dhahabu ambayo yamefanyika wilayani Kahama na kuhusisha washiriki 69.
Amefafanua kuwa moja ya lengo la mradi unaoendeshwa hivi sasa na shirika hilo ni kuwapa mafunzo wachimbaji wadogo waweze kuelewa jinsi ya kuboresha shughuli zao ikiwemo utunzaji wa mazingira.
Amesema Solidaridad hivi sasa inaleta wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa dhahabu kuanzia mchimbaji mpaka kwa mnunuzi wa kimataifa ili kutatua changamoto ambazo zipo kwa wachimbaji wadogo.
“Wadau hawawezi kuja mpaka wachimbaji tuhakikishe tumeboresha shughuli zetu, ndiyo maana tupo hapa kwa kushirikiana na Serikali, ofisi za madini, wadau mbalimbali na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kutoa elimu tuwafundishe muelewe vizuri na muweze kuboresha shughuli zenu,”ameeleza na kuongeza kuwa:
“Tutakuwa tunawatembelea mara kwa mara mpaka pale mtakapokuwa mmeelewa ili pindi mtakapokuwa mmeboresha shughuli zenu, tutawaunganisha na wadau wawaelewe, mfano wakifahamu mgodi wa Shigomiko wanazalisha vizuri, wanatunza mazingira, basi dhahabu yenu itakuwa na thamani ya kuuzwa popote duniani,”.
Kuhusu suala la usalama na uokozi migodini Mhandisi Kanwa amewataka wachimbaji kuhakikisha wanaunda timu za uokozi katika maeneo yao kwa lengo la kujali usalama wao na hivyo kuendesha shughuli za uchimbaji wenye tija unaozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake Mkaguzi wa migodi kutoka Ofisi ya Madini kimkoa wilayani Kahama, Mhandisi Gabriely Senge amewataka wakaguzi wote wa migodi midogo kuhakikisha wakati wote wanakuwa na daftari maalumu la kumbukumbu ya matukio yote ya ajali migodini.
Mhandisi Senge amesema ni muhimu wale wote watakaokuwa kwenye timu za uokozi wawe wakiyatambua pia mazingira ya matukio ya ajali pindi yanapotokea katika maeneo yao ili kunusuru pasitokea matukio mengine zaidi.
Sgt. Peter Francis ambaye ni Ofisa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga amewataka wakaguzi na mameneja wa migodi yote midogo kuhakikisha wananunua vifaa muhimu kwa ajili ya uokozi ili kuweza kusaidia kufanya uokozi ulio salama.
Kwa upande wao Mameneja na wakaguzi wa migodi kutoka migodi ya Mwime, Manda, Nyangalata na Kalole wamelishukuru Shirika la Solidaridad kwa elimu ambayo wameitoa kwao na kwamba jukumu lao hivi sasa ni kufanyia kazi yale yote ambayo wamefundishwa.
“Shirika la Solidaridad limetufundisha mambo mengi, japo tulikuwa na uzoefu fulani, lakini tumeongezewa elimu, mengi ni mfano wa mtu aliyekuwa kidato cha sita na sasa amefaulu kwenda Chuo Kikuu na sasa tumehitimu, yote haya tutayazingatia,”ameeleza Mboje Manyilizu kutoka mgodi wa Shigomiko na kuongeza
“Kikubwa tunaomba tuelekezwe maeneo ambayo tutaweza kupata vifaa hivi vya uokozi ili tuweze kwenda kuvinunua, mfano hiki kifaa cha kubaini kiwango cha gesi ndani ya duara, ni cha muhimu kwetu, maana tukikipata tutaachana na mfumo ule wa kutumia nyasi,”.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa