November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka mitatu ya Rais Samia na mageuzi makubwa sekta ya afya

Na Penina Malundo,TimesmajiraOnline,Dar

LEO Rais Samia Suluhu Hassan, anatimiza miaka mitatu tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, Watanzania wameshuhudia mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika sekta ya afya katika nyanja mbalimbali.

Mafanikio hayo yametokana na maono ya Rais Samia katika kuthamini afya za Watanzania.

Akizungumzia mafanikio ya Wizara ya Afya katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anasema katika kipindi cha miaka mitatu Sekta ya afya imepatiwa kiasi cha sh. Trilion 6.722 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali ili kuimarisha huduma za afya nchini.

Anasema Wizara ya Afya imetekeleza kwa mafanikio makubwa majukumu yake, ikijikita katika maeneo makuu mbalimbali yakiwemo; ujenzi wa Miundombinu ya Kutolea Huduma za Afya nchini, kuimarisha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya, Upatikanaji wa Huduma za Ubingwa na ubingwa Bobezi nchini.

Aidha, anasema imeweza kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa ikiwemo huduma za Mionzi, kuimarisha Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, kudhibiti maambukizi ya UKIMWI, Kifua KIkuu, Malaria na Magonjwa ya mlipuko, ajira kwa watumishi na ufadhili wa wanafunzi katika ngazi na fani mbalimbali pamoja na kupitishwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

***Ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma

Magari ya wagonjwa

Waziri Ummy anasema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita umefanyika uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kutolea huduma za afya ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,610 Machi 2024.
Anasema hiyo ni sawa na ongezeko la vituo 1,061. Pia anasema umefanyika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya

Waziri Ummy anasena Serikali imejenga na kufanya maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mipya mitano.

Maboresho hayo yamegharimu jumla ya Shilingi Trilioni 1.02 na yalifanyika katika maeneo yafuatayo;

Moja, Nyingine ni kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara na kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato. Hospitali hizi za Rufaa za Kanda zimeanza kutoa huduma katika miaka mitatu ya Uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan.

Mbili, kuendeleza ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa mipya mitano ambazo ni Katavi, Njombe, Songwe, Simiyu, Geita. Hospitali hizi zimeanza kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo husika

Tatu, kuhamisha Hospitali nne kutoka majengo yake ya zamani kwa kujenga Hospitali mpya katika maeneo mapya, Hospitali hizo ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Singida, Mara na Ruvuma,

Nne, Kukarabati na kujenga majengo mapya ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Ligula (Mtwara), Sekoutoure (Mwanza), Maweni (Kigoma), Sumbawanga (Rukwa) na Kitete (Tabora).

Tano, Ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri katika maeneo mbalimbali nchini kama ilivyoonyeshwa na OR-TAMISEMI

Sita, ujenzi wa mitambo 21 ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni kwa ajili ya wagonjwa mahututi na Wagonjwa wa dharura

UJUMBE MAHUSUSI: 

Anasema ongezeko la vituo vya kutoa huduma za afya nchini na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika yamewezesha kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi kama tunavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.

Waziri Ummy anasema hivi sasa asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za afya ndani ya kilometa 5 ya maeneo yao wanayoishi. Lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2030.

*** Kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa

Anasema katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa wagonjwa, Serikali ya Rais Samia imenunua vifaa Tiba vya Uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya sh.bilioni 290.9, ambavyo vinapatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa hadi Hospitali za Rufaa za Mikoa (RRHs) na Halmashauri.

Ummy anasema huduma za kipimo cha CT Scan sasa zinapatikana katika Hospitali 27 kati ya Hospitalii 28 za rufaa za Mikoa nchini. Kwa mwaka 2023, jumla ya wagonjwa 15,386 walipatiwa huduma za kipimo cha CT Scan katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo huduma hizo zilikuwa hazitolewi katika hospitali za Rufaa za Mikoa hapo awali.

**Vitanda vya kulaza wagonjwa

Ummy anasema idadi ya vitanda vya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeongezeka kutoka vitanda 86,131 mwaka 2021 hadi vitanda 126,209 Machi 2024. Ongezeko la vitanda vya wagonjwa limesaidia kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za afya hususani huduma za afya ya mama na mtoto.

Vilevile Serikali imekamilisha ujenzi wa wodi 45 za wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ngazi ya Taifa, Maalum, Kanda na Mkoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba.

Pia Serikali inaendelea na ujenzi wa ICU 28 katika ngazi ya Halmashauri ambapo 27 kati ya hizo zimekamilika na moja (1) iko hatua ya ukamilishaji. Hatua hii imeongeza idadi ya vitanda kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU) katika vituo vya umma kutoka vitanda 258 vya mwaka 2021 hadi kufikia vitanda 1,362 mwaka 2023.

Ummy anasema ongezeko la vitanda vya wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali za umma linalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kupunguza rufaa za wagonjwa wanaohitaji huduma za ICU kwenda katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Taifa na hivyo kupunguza msongamano wa wagonjwa sambamba na kupunguza vifo vinavyotokea ndani ya hospitali ambavyo vinaweza kuzuilika kati ya asilimia 20 hadi 30.

Kuiarisha upatikanaji wa dawa na bidhaa afya

Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa na bidhaa za afya ambapo, katika kipindi cha miaka mitatu, wastani wa Shilingi Bilioni 20 zimekuwa zikitolewa kila mwezi.

Upatikanaji wa fedha hizo umewezesha kuimarika kwa upatikanaji wa dawa muhimu na bidhaa nyingine za afya (aina 290) katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kufikia asilimia 84 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 58 mwaka 2022.

Aidha, hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya kwa ngazi za vituo vya kutolea huduma za afya hadi kufikia mwezi Desemba 2023 ni kama ifuatavyo;

Hospitali ya Kanda ya Chatoa

Upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi umehakikisha kila mwananchi anapata mahitaji yote muhimu ya msingi ya kimatibabu pale anapoenda kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Machi 2024, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika huduma za afya ya Uzazi, Mama na Mtoto. Uwekezaji huo umefanyika katika maeneo yafuatayo;

Kukamilisha ujenzi wa jengo la kutoa huduma za afya ya Mama na Mtoto Meta iliyopo katika Jiji la Mbeya ambayo tayari inatumika na imegharimu shilingi bilioni 13.2.

Kuendelea na ujenzi wa majengo ya huduma za Mama na Mtoto (Maternity Blocks) kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa ambazo ni Sekou Toure (Mwanza), Geita, Simiyu, Mawenzi, Njombe na Songwe ambazo zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 71.1.

Ummy anasema Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia imeimarisha huduma za upasuaji wa wajawazito kwa Kuongeza vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEMoNC) kutoka vituo 340 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 523 mwaka 2023.

Pia anasema imeanzishwa wodi maalum kwa ajili ya huduma za watoto wachanga wagonjwa (Neonatal Care Units – NCU), ambapo hadi kufikia desemba 2023 jumla ya Hospitali 189 zinatoa huduma za NCU ikilinganishwa na Hospitali 165 mwaka 2022 na Hospitali 14 tu mwaka 2018.

Nyingine kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ambapo upatikanaji wake katika Vituo vinavyomilikiwa na Serikali umeongezeka kutoka asilimia 82.5 mwaka 2021 hadi asilimia 88.2 mwaka 2023.

Pia kumeimarishwa huduma za Saratani ya mlango wa kizazi, ambapo jumla ya mashine 140 (Thermalcoagulator) za uchunguzi wa Saratani zimenunuliwa na kusambazwa kwenye vituo 140 vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri 104 katika Mikoa 26. Vifaa hivi vina thamani ya jumla ya shilingi Bilioni 1.1

Mfumo wa M-mama – Serikali ya Awamu ya Sita imeanzisha mfumo wa kieletroniki wa M-mama unaoratibu rufaa, kwa kusafirisha akina mama wajawazito na watoto wachanga wanaohitaji huduma za dharura kutoka ngazi ya jamii hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya au kutoka kwenye kituo cha kutolea huduma cha ngazi ya chini kwenda kituo cha ngazi ya juu.

Kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi mwaka 2023 mfumo huu umendelea kufanya kazi katika Mikoa yote 31 Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, jumla ya wateja 46,941 wamenufaika na huduma za dharura za rufaa, kati ya hao akina mama walikuwa 38,560 sawa asilimia 82, watoto wachanga walikuwa 8,273 sawa na asilmia 17 na mama pamoja na mtoto kwa pamoja walikuwa 108 sawa na asilimia moja (1). Vilevile, wateja wote wa m-mama wanahudumiwa na Watoa huduma waliopo kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya Serikali nchini. Mfumo huu umerahisisha utoaji wa huduma za dharura kwa wakati kwa kuwafikisha wateja katika vituo sahihi vya matibabu.

Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia katika kuimarisha ubora wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ambapo kupitia Viashiria vikuu vinavyotumika kupima mwenendo wa ubora wa huduma kwa Nchi Wanachama wa Shirika la Afya Duniani imejidhihirisha wazi kuwa Nchi yetu imefanya vizuri sana katika kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika kipindi cha miaka mitatu.

Matokeo ya baadhi ya viashiria hivyo ni pamoja na ongezeko la wajawazito waliojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya idadi ya wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeendelea kuongezeka kutoka asilimia 63 mwaka 2021 hadi asilimia 85 mwaka 2023.

Lengo la nchi ni kufikia asilimia 95 ya wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ifikapo mwaka 2030.

Wamepunguza vifo vya wanawake wajawazito kwa asilimia 80 – Kuimarika kwa huduma za uzazi, mama na mtoto kumepelekea kupunguza vifo vya wajawazito vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa .

vifo vya watoto umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022.

Vifo vya watoto umri chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 33 kwa kila vizazi hai 1,000 hadi sasa,

Vifo vya watoto wachanga (wenye umri wa chini ya siku 28) vimepungua kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi vifo 24 kwa vizazi hai 1,000 hadi sasa.

***Kuimarisha upatikanaji huduma za kibingwa

Serukali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi mahirii wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi (Specialized and Super Specialized) ikiwemo huduma za Upasuaji mgumu wa moyo bila kufungua kifua (Cathetarization procedure), Upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo; upandikizaji Figo (Kidney Transplant), Upandikizaji Uloto (Bonne Marrow Transplant); Upandikizaji wa Vifaa vya Usikivu kwa watoto (Cochlea implants), kuweka puto tumboni na upasuaji mgumu wa mifupa na mishipa ya fahamu.

Katika kipindi cha miaka mitatu, Huduma za Ubingwa Bobezi zilizotolewa zilikuwa ni pamoja na;-

Upandikizaji vifaa vya usikivu kwa watoto ambapo jumla ya watoto 25 waliowekewa kati ya hao watoto 11 wamewekewa vifaa hivyo mwaka 2023/24

Upandikizaji wa figo ulifanyika kwa wagonjwa 27, kati yao wagonjwa 16 wamefanyiwa katika kipindi cha mwaka 2023/24
Upandikizaji uloto wagonjwa15 tangu ilipoanzishwa mwaka 2021.

Upasuaji wa Moyo kwa njia ya Tundu dogo wagonjwa 5,954 kati yao wagonjwa 2,289 wamefanyiwa katika kipindi cha mwaka 2023/24,

Kuweka Goti Bandia wagonjwa 662, kati yao wagonjwa 385 wamefanyiwa katika kipindi cha mwaka 2023/24,

Kuweka puto tumboni wagonjwa 166 wamepata huduma hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 na

Huduma hizi ziliolewa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI); Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa (MOI); Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na Hospitali nyingine za Rufaa za Kanda na Mikoa.

Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha huduma ubingwa na ubingwa bobezi umewezesha wananchi wengi kupata huduma hizi ndani ya nchi kwa gharama nafuu badala ya kuzitafuta nje ya nchi.

Aidha uwekezaji huu umeweza kuvutia wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa Kituo cha Tiba Utalii kwa ukanda wa nchi za afrika mashariki na kusini mwa afrika.

Tiba Utalii nchini inakuwa, tunashuhudia ongezeko la Raia wa kigeni kuja Tanzania kwa ajili ya matibabu.

Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma za kibingwa na bobezi, nchi yetu imeweza kuvutia wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Kwa mwaka 2023, idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi wa Tiba Utalii waliokuja kutibiwa nchini ilikuwa 6,931 ikilinganishwa na wagonjwa 3,957 mwaka 2022 na wagonjwa 75 mwaka 2021. Wagonjwa hawa wanatoka katika nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Congo DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenya.

Wagonjwa hawa walihudumiwa katika Hospitali 6 ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI) na Hospitali binafsi za Aga khan na Saifee

Serikali ya Rais Samia kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi na wananchi. Kupitia Mafunzo elekezi kutoka kwa wataalam bingwa (Mentorship Program) kutasaidia kuleta chachu ya mabadiliko ya utoaji huduma za afya ili kuweza hudumia vyema wananchi katika kupata huduma bora za kibingwa

***Kuimarisha huduma za dharura za ajali

Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha ujenzi wa majengo 23 ya kutoa huduma za dharura (EMD) katika hospitali Maalum, Kanda na Mikoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba. Aidha kwa upande wa ngazi ya msingi, ujenzi wa EMD 82 katika ngazi za Halmashauri unaendelea, ambapo EMD 66 zimekamilika na zinatoa huduma na nyingine 16 ziko kwenye hatua ya ukamilishaji.

Miaka mitatu ya Rais Samia imewezesha kuanzishwa kwa majengo mahususi ya huduma za dharura na ajali (EMDs) 105 kutoka EMD 7 zilizokuwepo mwaka 2020. Aidha, hadi sasa jumla ya wateja 262,260 wamenufaika na huduma za dharura nchini.

Kukamilika kwa ujenzi wa EMD kutapunguza vifo na kuokoa maisha kwa wagonjwa wa dharura na wa ajali kwa asilimia kati ya 40-50 kwa mujibu wa tafiti za kitaalam.

Kukamilika kwa ujenzi wa EMD kumeongeza idadi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, maalumu, na kanda zinazotoa huduma hiyo kutoka 7 mwaka 2020 na kufikia 116 Desemba 2023. Yote haya yamepatikana ndani ya miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Matokeo ya uwezekaji huu kutapunguza vifo ndani ya hospitali kwa asilimia 40 na kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma za dharura na ajali.

***Magari ya kubebea wagonjwa yanunuliwa na kusambazwa kila kona

Pia, Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 727 ambapo hadi sasa jumla ya 327 yamepokelewa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Ambulance hizi zinakwenda kusaidia kusafirisha wagonjwa wakiwemo akinamama wenye changamoto za uzazi kwa haraka na kuwafikisha katika huduma za rufaa na hivyo kupunguza adha kwa wananchi na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

***RAsilimali watu katika sekta ya afya

Serikali ya Awamu ya sita imeendelea kufanya uwekezaji katika eneo la rasilimali watu katika afya ikiwemo kuajiri watumishi wapya wa Sekta ya Afya na kusomesha wataalamu wa afya katika fani mbalimbali za ubingwa na ubobezi.

Serikali imeendelea kuajiri wataalam katika Sekta ya Afya ambapo jumla ya wataalam 35,450 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2023. Aidha, jumla ya ajira za mikataba kwa watumishi wa Afya 2,836 kupitia miradi mbalimbali ya Serikali zilitolewa.

Ongezeko la Madaktari bingwa na bobezi, ambapo jumla ya madaktari bingwa nchini hadi kufikia mwaka 2023 wamefikia 2,464 ukilinganisha na madaktari Bingwa 805 mwaka 2020.

***Uendelezaji wa Rasilimali Watu katika Afya

Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha upatikanaji wa wataalam wabobezi kwa ajili ya utoaji wa huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi, kwa kuanzisha Dkt Samia Super Specilized Scholarships ambapo hadi sasa, jumla ya wataalam 1,211 wamepata mafunzo mbalimbali ya kibingwa na bobezi na hivyo kuongeza idadi ya wataalam wa mafunzo ya kibingwa na bobezi kutoka 535 mwaka 2021 hadi 1,211 hadi kufikia sasa.

Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 22 kimetumika kugharamia mafunzo haya.

Jitihada hizi zitasaidia kupata wataalam wa afya kwenye fani za kibingwa na bobezi watakaotumika kujenga uwezo wa wataalam wetu wa afya katika vyuo vya mafunzo ya afya nchini.

Vilevile jitihada hizo zitaimarisha upatikanaji wa huduma hizo za kibingwa bobezi ambazo zitawezesha nchi kunufaika na tiba utalii. Hadi sasa Taasisi zetu zimeweza kutoa tiba utalii kutoka nchi za Comoro, Burundi, Malawi, Kenya, Congo DRC, Uganda na Zambia.

Kwa upande wa ugonjwa wa UKIMWI, Serikali imeendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI ambapo katika mwaka 2023 jumla ya watu 8,145,576 walipima Virusi vya UKIMWI (VVU) kulinganisha na watu 6,930,758 mwaka 2022 na watu 6,493,583 mwaka 2021 (Taarifa kutoka Mfumo wa DHIS2 2023).

Kati ya watu waliopima mwaka 2023, watu 163,131 walingundulika kuwa na maambukizi ya VVU ukilinganisha na watu 182,095 mwaka 2022 na watu 198,042 mwaka 2021 (DHIS2 2023).

Waliokuwa wanatumia dawa za kufubaza virusi vya VVU walikuwa 1,663,651 Desemba 2023 kulinganisha na watu 1,612,512 Desemba 2022 na watu 1,520,589 mwaka 2021. Mwaka 2023, Vifo vitokanavyo na UKIMWI vilikuwa 22,000 kulinganisha na vifo 29,000 mwaka 2022 na vifo 25,000 mwaka 2021 (Spectrum 2022).

Katika kuhakikisha kuwa huduma kwa WAVIU zinasogezwa karibu zaidi na jamii, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa maendeleo imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kabisa za kuhakikisha kila kituo cha afya nchini kinakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa waathirika wa UKIMWI.

Hadi kufikia Mwezi Desemba 2023, Idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya Tiba na Matunzo vimefikia vituo 7,396 kutoka vituo 7,072 mwaka 2021 na kati ya hivyo CTC kamili ni 3,572 na vituo vya huduma ya mama na mtoto (RCHS) vinavyotoa huduma ya kutoa dawa ya kufubaza Virusi vya UKIMWI vipo 3,824.

Kwa upande wa ugonjwa wa MALARIA, Serikali imeendelea kudhibiti maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria ambapo katika mwaka 2023 jumla ya watu milioni 19.8 walipima ugonjwa wa Malaria kati yao watu milioni 3.46 walikutwa na Malaria kulinganisha na watu milioni 18.6 walipima mwaka 2022 na kati yao milioni 3.52 walikutwa na ugonjwa na watu Milioni 20,241,982, waliopimwa mwaka 2021 na kati yao Milioni 4,443,946 walikutwa na maambukizi. Vifo vitokanavyo na Malaria vilikuwa 1,540 mwaka 2023 ukilinganisha na vifo 1,735 mwaka 2022 na vifo 1,882 mwaka 2021.

Kwa upande wa ugonjwa wa Kifua Kikuu, Serikali iliendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu ambapo katika mwaka 2023 jumla ya watu 440,988 walipima ugonjwa wa TB kulinganisha na watu 398,676 mwaka 2022 na watu 354,324 mwaka 2021.

Waliogundulika kuwa na TB mwaka 2023 ni 90,585 kulinganisha na watu 100,984 mwaka 2022 na watu 60,068 mwaka 2021. Mwaka 2023, Vifo vitokanavyo na TB vilikuwa 18,100 kulinganisha na vifo 25,800 mwaka 2022 na vifo 26,800 mwaka 2021.

***Udhibiti wa magonjwa wa mlipuko

Mwaka 2023, visa vya viwili vya ugonjwa wa Marburg vilipatikana, ambapo Serikali iliweza kudhibiti kabisa kusambaa kwa ugonjwa hatari wa Marburg kwa kupitia uwekezaji wa miundombinu ya maabara ya kisasa Mkoani Kagera, nchi yetu iliweza kupambana na janga la Marburg kwa kugundua mapema na kuudhibiti ndani ya siku 69 hii ikiwa ni historia ukilinganisha na nchi za jirani kama Uganda iliyotumia siku 113 na Equtorial Guinea siku 122.

Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na. 13 ya mwaka 2023 ambapo tarehe 19 Novemba, 2023 iliwekwa saini na Dkt. Samia.

Malengo makuu ya Sheria ya bima ya afya kwa wote ni kuwawezesha wananchi wote kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya wakati wote bila kikwazo cha fedha hususan kwa kaya masikini.

Aidha, mafanikio ya kutungwa kwa Sheria hiyo pia ni kuanzishwa kwa mfuko wa kugharamia bima ya afya kwa kuwa na vyanzo mahususi vya fedha.

Mfuko huo utawezesha wananchi wasio na uwezo kunufaika na huduma za afya kwa uhakika ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa. Vilevile kutekelezwa kwa Sheria hiyo kutawezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na mapato ya uhakika na hivyo kuboresha huduma za afya zitolewazo kwa wananchi.

Miaka mitatu ya Uongozi wa Dkt Samai Suluhu Hassan, sekta ya afya inasonga mbele. Namba zinaongea.

Tunamshukuru Raisi kwa maono yake na kwa kutuwezesha kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za afya. Aidha tunawashukuru na kuwapongeza watumishi wa afya wa kazi zote kwa kuhudumia wananchi.

Vilevile tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mzuri katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini. Tunatoa wito kwao kuchukua hatua ili kujikinga na kudhibiti magonjwa ya kuambikiza na yasiyo ya kuambukiza.

Wizara itaendelea kuchukua hatua mahususi ili kutatua changamoto zilizopo na zitakazojitokeza katika utoaji wa huduma za afya.