November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaboresha mazingira ya uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Dar

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida, amasema serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa ya Kisera na Kisheria ili kujenga mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji nchini.

Dkt. Kida, amesema hayo juzi jijini Dar es Salaam alipofanya kikao na Joy Basu, Makamu Msaidizi wa Shughuli za Serikali ya Marekani, Ofisi ya Ustawi wa Biashara Afrika, kwa niaba ya Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.

“Tunafanya maboresho ya kisera na sheria zetu, na tunatunga mpya nyingine ili kuondoa vikwazo kwa wawekezaji” amesema Dkt. Kida.

Maboresho hayo, yanakwenda sambamba na kuhamisha mfumo wa analojia ambao awali ulimtaka mwekezaji kutembelea taasisi zaidi 10 ili kukamilisha taratibu za kuwekeza nchini.

“Tumetengeneza mfumo wa kidigitali wa Dirisha la Mahali Pamoja (TeIW), mfumo huo unajumuisha taasisi saba,na tunafanyia kazi taasisi nyingine tano, ili kumwezesha mwekezaji kukamilisha taratibu mbalimbali za uwekezaji kwa njia ya kidigitali, kwa kuwa mifumo hiyo inasomana”.

Akibainisha maboresho mengine makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Kida ameeleza kuwa ni kuundwa kwa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji inayojumuisha taasisi nne ambazo ni; Tume ya Mipango, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Kituo cha Uwekezaji (TIC), na Mamlaka ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA), hatua inayorahisisha uratibu wa shughuli za Mipango na Uwekezaji nchini .

“Tumefanya maboresho mengi na tunaendelea, nina hakika ndani ya muda mfupi vikwazo vingi vitakuwa vimeshughulikiwa kwa kiwango kikubwa, na hivyo kuwapa uhakika zaidi wawekezaji” amesema, Dkt. Kida.

Kwa upande wake Joy Basu, alisema nia yao ni kuona namna gani Tanzania na Marekani zitaongeza ushirikiano wenye tija katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji nchini.

Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri amefanya wasilisho la fursa mbalimbali za kiuwekezaji, maeneo mahususi ya fursa hizo, kiwango cha mitaji, vigezo vya kuwekeza, na motisha za kuwekeza nchini.

Tangu mwaka 1997 hadi 2023, miradi zaidi ya 296 ya uwekezaji wenye ushirika wa Marekani imesajiliwa nchini, na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi ziizosajili miradi mingi nchini kupitia TIC.