November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shangazi ataka mbegu za ngano zisigawiwe kisiasa

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Mlalo, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Rashid Shangazi ametaka mbegu za zao la ngano zisigawiwe kisiasa bali zigawiwe kwa kulenga tija kwa mkulima ili aweze kupata mazao yatakayomuinua kiuchumi.

Ameyasema hayo Februari 25, 2024 wakati akigawa kwa wakulima wa Jimbo la Mlalo tani 100 za mbegu za ngano kwenye hafla iliyofanyika Kijiji cha Mnadani, Kata ya Malindi ambayo ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge, Madiwani,Watendaji wa Kata na maofisa ugani.

Mbunge wa Jimbo la Mlalo (wa pili kulia) akikabidhi mfuko wa mbegu ya ngano kwa Ofisa Mtendaji Kata ya Mtae Miraji Msagati (wa pili kushoto)

Shangazi amewataka Madiwani na Watendaji wa Kata kugawa mbegu hizo kwa tija huku maofisa ugani wakitakiwa kuwa makini na kuwashauri vizuri wakulima namna bora ya kulima, kupanda na kuvuna kwa tija pamoja na kiwatembelea mara kwa mara kwa ajili ya kutoa ushauri.

“Nafarijika kuona tani 19 za mbegu (mwaka jana) zilizaa tani 300, nitafarijika kuona kwa usimamizi na ushirikishwaji wa wakati huu, tani 100 zikizalishwa hadi tani 10,000,tutakuwa tumetenda jambo jema,naataka watendaji na maofisa ugani mjiamini, na hasa maofisa ugani mjiamini sana kama kuna jambo jipya semeni tutakuja,” amesema Shangazi.

Mbunge wa Jimbo la Mlalo Rashid Shangazi (wa pili kulia) akimkabidhi mfuko wa mbegu ya ngano Diwani wa Kata ya Malindi, Msumba Mngumi (wa tatu kushoto), Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge, na wa tatu kulia ni Kaimu Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto George Medeye.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Lushoto,Ikupa Mwasyoge ameeleza kuwa wameanza kupata matokeo makubwa kwenye kilimo hivyo amempongeza Shangazi kwa kazi anazofanya, kwani mbegu hizo alizopeleka kwa wakulima kutoka Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA), hakugawa kwa wakulima wa Jimbo la Mlalo tu, bali hata Jimbo la Lushoto wamepeleka tani 20.

Kaimu Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto George Medeye amesema zao la ngano lilikuwa linalimwa siku za nyuma kwenye Wilaya ya Lushoto lakini kutokana na kuyumba kwa soko, na wananchi kulima mazao mengine, zao hilo halikuwa na tija.

Mbunge wa Jimbo la Mlalo (wa pili kulia) akikabidhi mfuko wa mbegu ya ngano kwa Diwani wa Kata ya Mlalo Rashid Rajab ‘Madagaa’ (wa tatu kushoto).

Lakini kwa sasa zao hilo ni muhimu kwa Wilaya hiyo sababu lina soko ndani na nje ya nchi na kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mahindi hayastawi vizuri hivyo ngano itakuwa mkombozi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge akizungumza kwenye hafla ya kugawa mbegu ya ngano kwa Madiwani na Watendaji Kata Jimbo la Mlalo iliyofanyika Kijiji cha Mnadani, Kata ya Malindi.
Sehemu ya shehena ya mbegu ya ngano ikiwa kwenye ghala Kijiji cha Mnadani, Kata ya Malindi.