Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
ILI kumaliza malalamiko kwa abiria wanaosafiri masafa marefu Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) kimewakutanisha watoa huduma 70 wa Kanda ya Kati wanaohudumia mabasi ya Masafa Marefu na kuwapatia Mafunzo ya muda mfupi kupitia mradi wa East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP)uliofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo jiji hapa leo,Februari 12,2024 Mkuu wa Idara ya Usalama katika Usafirishaji na Uhandisi wa Mazingira-NIT,Patrick Makule amesema mafunzo ya wahudumu wa mabasi ya Masafa Marefu na Mijini Kanda ya Kati-Tanzania yanalenga kuwafunza watoa huduma hao kutoa huduma iliyobora kwa wateja wake.
Ameeleza kuwa kuwepo kwa Mafunzo hayo ya siku tano ni mchakato wa muda Marefu na ni muhimu kwa watoa huduma kuyapata kwani kumekuwepo na malalamiko kwa abiria.
“Tumeona kunauhitaji mkubwa wa kuhakikisha watoa huduma kwenye mabasi wanapatiwa mafunzo ili wasafiri waweze kufurahia safari zao lakini pia kumaliza malalamiko yanayoendelea kwa sasa,”amesema Makule.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA) Mkoa wa Dodoma,Ezekiel Emanuel amesema Mafunzo hayo yataleta mapinduzi chanya kwenye sekta ya usafirishaji kwani wao
wamekuwa na jukumu la kutatua migogoro wakipokea malalamiko kutoka kwa wapokea huduma ambao ni abiria.
“Watoa huduma kwenye mabasi ya Masafa Marefu wamekuwa wakitoa huduma iliyochini ya kiwango na hiyo yote ni kutokana na kutokuwa na elimu sahihi ya huduma kwa mteja,
“Hivyo niwaombe wamiliki wa magari ya usafirishaji wajitahidi kuwapeleka watoa huduma kupata Mafunzo ya huduma kwa wateja kwani kwakufanya hivyo itawasaidia kwenye biashara zao,”amesema.cha
Mkuu wa kitivo cha mafunzo ya lojistiki na biashara Dkt. Prosper Nyaki amesema Kozi hiyo ya muda mfupi itawajengea washiriki uwezo na umahiri katika kuzitambua Sheria za LATRA na Kanuni zake, utoaji wa huduma bora kwa mteja,mbinu za utoaji wa huduma ya kwanza,usalama wa abiria na mali zao, utunzaji wa mizigo na utambuzi wa
bidhaa hatarishi kwa kuzingatia kanuni za usafirishaji, namna bora ya kushughulikia malalamiko ya mteja, usafi na utunzaji wa
mazingira, mahusiano na mawasiliano, nidhamu na unadhifu wa mtoa huduma, pamoja na maarifa ya utoaji na umuhimu wa tiketi mtandao.
“Mgeni Rasmi,Mafunzo haya ni endelevu na yatakua yakiendeshwa katika Kampasi ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji iliyopo Mabibo,jijini Dar es Salaam kwa muda wa wiki mbili na gharama nafuu kwa kila mshiriki (kalenda ya mafunzo hayo pamoja na gharama inapatikana katika
tovuti ya Chuo ambayo ni www.nit.ac.tz).
Aidha amesema kuwa Chuo kipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za
mashirikiano na VETA ambapo kupitia mashirikiano hayo Chuo kitasogeza huduma zaidi kwa wadau kupitia kampasi za Vyuo vya VETA ambavyo vipo katika kanda zote za Tanzania.
Ameeleza kuwa Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa katika nchi tatu yaani Tanzania, Kenya na Ethiopia ili kuwezesha muingiliano wa
kijamii katika nchi za ukanda wa Afrika.
Amefafanua kuwa katika kufikia malengo ya Mradi, Chuo kina majukumu ya Kuandaa Mitaala inayokidhi matakwa ya soko la ajira, kuongeza ushirikiano na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi
kwa kuwa na mikataba ya ushirikiano , Kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ,Kuzifikia Taasisi zingine ambazo ziko nje ya mradi na kutoa mafunzo ,Kuwajengea uwezo
watumishi katika nyanja mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Hivyo basi, katika kutekeleza malengo hayo ya mradi wa EASTRIP hususani lengo Na. IV, Chuo kimeandaa mafunzo haya kufanyika katika Kanda sita za Tanzania ambapo washiriki watakaopata udahili
katika kanda hizo watalipiwa ada ya mafunzo kupitia fedha za Mradi.
Kabla ya kufungua mafunzo hayo,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema
kuwa,kuwepo kwa mafunzo hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia waliowezesha kuwepo kwa Mradi huo wa EASTRIP unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambao ni mkopo wa Serikali.
Hata hivyo ameupongeza Uongozi wa Chuo, wanataaluma na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanafanyika katika Mkoa wa Dodoma kwa kanda hii ya Kati kwani wangeweza kuamua yakafanyika mikoa mingine ya kanda hii, kwa Dodoma ni heshima kubwa.
“Ombi langu kwa Chuo ni kuhakikisha kinatoa mafunzo haya mara kwa mara ili wataalamu hawa waendelee kutoa huduma zinazo kidhi vigezo kwa wateja wao,nina hakika, ikiwa kila mmoja atatekeleza majukumu yake na kuyafanyia kazi yote niliyoyataja pamoja na mengineyo natumaini kwamba malalamiko ya wateja wenu yatapungua kwani ni muhimu kuzingatia yale mtakayojifunza ndani ya siku tano (5) hapa,”amesema Senyamule.
Amesema ili kuweza kufanikiwa ni lazima kila mmoja aweze kusoma kwa bidii na kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi