October 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabaki ya mkonge kuzalisha chakula, mbolea

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tanga

MABAKI ya mkonge yanayozalishwa kwa wingi katika viwanda vya uchakataji wa zao hilo hapa nchini yanaweza kugeuzwa na kuwa chakula cha mifugo chenye protini nyingi, mbolea hai na nishati, hatua inayofungua fursa mpya za kiuchumi huku ikipunguza changamoto za utunzaji wa mazingira.

Matokeo ya utafiti yaliyowasilishwa jana, yanaonesha kuwa mabaki hayo, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakichukuliwa kama taka za viwandani, yanaweza kuongezewa thamani na kutumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye manufaa katika sekta za kilimo, ufugaji na nishati.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri na Mtafiti kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, Dkt. Aziza Konyo amesema,utafiti huo ulilenga kutafuta njia mbadala za kutumia mabaki ya mkonge yanayozalishwa kwa wingi viwandani lakini hayatumiki kikamilifu.

Amesema, katika uzalishaji wa nyuzi za mkonge,takribani asilimia nne hadi sita tu ya malighafi inayogeuzwa kuwa nyuzi nyeupe, huku sehemu kubwa iliyobaki ikihitaji kutafutiwa matumizi yenye tija badala ya kuendelea kuwa taka.

“Katika utafiti wangu nililenga kutatua tatizo la uzalishaji wa taka nyingi katika viwanda vya mkonge kwa kutumia mabaki hayo kuzalisha chakula cha mifugo chenye protini nyingi na mbolea isiyo na kemikali za viwandani,” amesema Dkt.Konyo.

Amefafanua kuwa katika kutekeleza utafiti huo, watafiti walitumia teknolojia ya nzi aina ya Black Soldier Fly, ambao mabuu yake hulishwa mabaki ya mkonge na kuvunwa baada ya siku 14 hadi 18.

Kwa mujibu wa mtafiti huyo, mabuu hayo hukusanywa,kukaushwa na kutumika kama kiungo cha chakula cha mifugo chenye protini nyingi, huku mabaki yanayobaki baada ya mchakato huo yakitumika kutengeneza mbolea hai.

Pia amesema, mbolea hiyo inaweza kusaidia kurejesha rutuba ya udongo na kuongeza virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mimea vikiwemo  nitrojeni, fosforasi na potasiamu (NPK), kwa mujibu wa vipimo vya maabara vilivyofanyika katika utafiti huo.

Utafiti huo unaonesha uwezekano wa kutumia teknolojia zinazobadili mabaki ya uzalishaji kuwa malighafi ya bidhaa nyingine, hali inayoweza kupunguza upotevu wa rasilimali na kuongeza thamani ya zao la mkonge kuanzia shambani hadi viwandani.

Kwa upande wake, Mtafiti kiongozi wa mradi huo kutoka Chuo cha Nelson Mandela, Profesa Anthony Mshandete amesema,utafiti huo ni sehemu ya juhudi za kutafuta matumizi yenye tija kwa mabaki ya mazao ya kilimo yakiwemo mkonge na kahawa, kupitia teknolojia za kuongeza thamani.

Amesema mradi huo unahusisha Tanzania, Kenya, Ethiopia na Denmark ukiwa na lengo la kuchunguza namna mabaki ya mazao yanavyoweza kutumika kuzalisha bidhaa nyingine na kuchangia maendeleo ya kilimo na viwanda.

Prof.Mshandete amesema,watafiti pia wanachunguza uwezekano wa kuzalisha nishati kutokana na mabaki ya mkonge yanapochanganywa na mabaki mengine ya kilimo, pamoja na kuboresha teknolojia zitakazowezesha uzalishaji huo kufanyika kwa njia endelevu na rafiki kwa mazingira.

Ameongeza kuwa utafiti huo unahusisha pia uchunguzi wa matumizi ya mbao zinazotokana na mkonge kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali, huku watafiti wakitathmini masuala ya kimazingira na mahitaji ya kiteknolojia kabla ya uwekezaji mkubwa kufanyika.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Saddy Kambona amesema,bodi hiyo inaendelea kushirikiana na watafiti katika kutafuta njia za kuongeza thamani ya mkonge na kuhakikisha mabaki yanayotokana na uchakataji wake yanakuwa sehemu ya fursa mpya za kiuchumi katika sekta hiyo.

“Matokeo ya tafiti zinazolenga kuongeza thamani ya mkonge ni muhimu katika kutafuta matumizi mapya ya zao hilo, ili sekta iweze kunufaika zaidi na bidhaa zinazozalishwa pamoja na mabaki yanayotokana na uchakataji wake,” amesema Kambona.

Utafiti huo unatoa mwelekeo mpya wa matumizi ya mabaki ya mkonge, ambapo badala ya kuyaona kama taka zisizo na manufaa, yanaweza kuwa malighafi muhimu katika uzalishaji wa chakula cha mifugo, mbolea hai na nishati, huku yakichangia kupunguza changamoto za kimazingira na kuongeza thamani ya zao hilo nchini.