October 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbeya UWSA yatii agizo la Waziri Aweso

Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline, Mbeya

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mbeya (Mbeya UWSA) imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji, Mh. Jumaa Aweso, la kuwaunganishia maji kwa mkopo wananchi wa Inolo na Uyole baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Savyutusu.

Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki wakati Makamu wa Rais, Mh. Deogratius Ndejembi, alipokuwa mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi, ambapo akiwa katika Jimbo la Uyole alimpa nafasi Waziri wa Maji kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya maji. Waziri alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na hivyo kuagiza Mamlaka ya Maji kuwaunganishia maji kwa mkopo.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 20, 2026 na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Neema Mwangwala, wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo katika eneo la Inolo

Mwangwala amesema kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira tayari imeanza kutoa huduma ya maji kwa kuwaunganisha wateja kwa utaratibu wa mkopo ambao utamwezesha mteja kupata huduma ya maji bure huku akiingia mkataba wa kulipa deni la maji kwa miezi mitatu.

“Utaratibu huu unalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi kwa urahisi zaidi bila kulazimika kulipa gharama za awali kwa awamu moja kama ambavyo ilizoeleka. Tunaamini huduma hii itamkomboa mpaka mwananchi wa chini,” amesema Mkurugenzi huyo.

Pia Mwangwala amewataka wananchi kuwa makini na kuepuka kutoa fedha taslimu kwa mtumishi yeyote wa Mamlaka kwa ajili ya malipo ya huduma za maunganisho mapya ya maji, na kueleza kuwa malipo yote yanapaswa kufanyika kupitia namba ya malipo (Control Number) inayotolewa na Mamlaka.

Aidha, Mamlaka imewahimiza wakazi wa Inolo kutumia fursa hiyo ya maunganisho mapya ya majisafi kwa kufuata taratibu zilizowekwa ili kuepuka usumbufu.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi wa Kata ya Inolo, Neema Aloyce, ameshukuru Mamlaka ya Maji kwa utaratibu huo walioweka na kueleza kuwa utasaidia kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa Inolo na Uyole, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji safi na salama.

“Tunamshukuru Waziri wa Maji na uongozi mzima wa Mamlaka ya Maji kwani wengi wetu tulikuwa tunapata shida sana ya maji, lakini kwa uamuzi huu shida ya maji sasa imeisha. Tutahakikisha tunalipa fedha kwa wakati ili tuendelee kupata huduma,” amesema.