Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar
ZAIDI ya wanafunzi 20 wa darasa la tatu kutoka shule ya msingi ya Reader Rabbit Bay Bridge, iliyopo jijini Dar es Salaam wamefika Makumbusho ya Taifa ya Jiolojia Tanzania ili kujifunza jiolojia ya miamba na madini yapatikanayo nchini hapa na Afrika kwa ujumla.
Mafunzo hayo yametolewa Januari 31, 2024 na Wataalamu wa Makumbusho hayo kutoka taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) baada ya wanafunzi hao kutembelea makumbusho hayo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwalimu wa shule hiyo ambaye pia ni kiongozi wa timu, Ringo Iringo, amefurahishwa na aina za miamba na madini yaliopo kwenye Makumbusho hayo ambapo amesema wanafunzi wake wamejifunza mengi kuhusina na jiolojia ya miamba na madini yapatikanayo Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Sambamba na hayo, Iringo amesema, wanafunzi wake wamejifunza jiolojia ya Tanzania, Afrika na ulimwengu mzima kwa nadharia hivyo uongozi wa shule hiyo ukaona umuhimu wa kufika Makumbusho ili kujifunza kwa vitendo.
Kwa upande wake, Kaimu Msimamizi wa Makumbusho hayo, Andrew Buluba, ameipongeza shule hiyo kufika katika Makumbusho hayo kujifunza jiolojia ya miamba na madini ambapo amesema elimu hiyo itawasaidia katika masomo yao hususani somo la Jografia.
Naye, Mjiolojia kutoka GST, Berther Matobango, ametoa wito kwa shule nyingine kutembea Makumbusho hayo kwa lengo la kujifunza jiolojia ya miamba na madini yapatikanayo Tanzania, Afrika na ulimwenguni kote.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Kanzi Data ya Taifa ya Jiolojia kutoka GST, Renata Bitumbiko amesema, Makumbusho ya Taifa ya Jiolojia Tanzania yalianzishwa na Mamlaka ya Utawala wa Makoloni ya nje ya Serikali ya Kikoloni ya Muingereza kwa lengo la kukusanya na kuhifadhi sampuli za miamba na madini ili kusaidia kuonesha aina za madini zilizopo katika himaya fulani na kusaidia wataalamu kufanya marejeo.
Akitoa maelezo kuhusu Makumbusho hayo, Mjiolojia kutoka GST, Mustadi Shabani amesema Makumbusho hayo yalikusudia kuonesha jiolojia na rasilimali madini iliyopo nchini na kuwapa mwelekeo wachimbaji na watafutaji wa madini katika maeneo mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha