November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kushusha gharama za uletaji mafuta

-Dkt. Biteko asema gharama ya mafuta ni nafuu kulinganisha na nchi jirani

-Asema kampuni ya mafuta TANOIL inaboreshwa ili kuleta ufanisi

-Asisitiza PBPA ni nguzo ya Serikali katika uhakika wa upatikanaji mafuta

-PBPA yazidi kudhibiti upotevu wa mafuta

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, juhudi zinazofanywa na Wizara ya Nishati, Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zimepelekea gharama za uletaji wa mafuta nchini (premium) kuendelea kushuka na hivyo kuleta unafuu wa gharama za mafuta ikiwemo ya dizeli na petroli.

Amesema hayo Januari 19,2024 jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha taarifa kuhusu mwenendo wa biashara ya mafuta nchini kwa kipindi cha mwezi Septemba hadi Disemba 2023, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Kikao ambacho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati,Judith Kapinga, Katibu Mkuu, Mhandisi, Felchesmi Mramba, baadhi ya Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara na Watendaji wa Wizara ya Nishati.

“ Wizara ya Nishati, EWURA na PBPA, kwa kweli wamefanya kazi kubwa ya kushusha gharama za uagizaji mafuta kutoka nje ya nchi, hapo awali gharama hizi zilikuwa zikiongezeka kila mwezi lakini wamesimamia vizuri suala hili na gharama hizi zimeanza kushuka na hivi karibuni mlisikia Waziri wa Kenya akisema bei za mafuta nchini humo zipo juu na za Tanzania zipo chini sababu ya premium, na wengine pia walio nje wanatoa ushuhuda kwamba walau sisi gharama zetu zina unafuu,”amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa PBPA ambayo inasimamia uagizaji wa mafuta kwa pamoja ina umuhimu mkubwa nchini kwani ndiyo inayopelekea nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaohitajika.

Na Serikali kufahamu kiwango cha mafuta kinachoingia nchini, kupanga ukusanyaji wa mapato kwa kutumia takwimu sahihi na kupanga bei elekezi ya mafuta.


Amesema kuwa, Serikali itaendelea kuisimamia kwa ukamilifu taasisi hiyo ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi kwani tayari imekuwa ni mfano wa kuigwa kwa nchi zinazotuzunguka na kuwataka watendaji wake kufanya kazi kwa maadili bila kumuonea mtu yeyote.

Vilevile ameeleza kuwa,serikali inaendelea kuiboresha kampuni ya mafuta ya TANOIL ambayo ni kampuni tanzu ya TPDC kutokana na umuhimu wake katika biashara ya mafuta nchini.

Na kwamba, TANOIL imekuwa kimbilio hasa katika nyakati ambapo zinatokea changamoto za upatikanaji mafuta kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi ameeleza kuwa, ili kuboresha mfumo wa upakuaji mafuta melini na kuhakikisha kuwa meli hazikai muda mrefu bandarini, Serikali iliagiza matenki ya TIPER nayo yatumike kupokea na kuhifadhi mafuta.

Ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo imewezesha meli za mafuta ya dizeli kutumia siku nne kushusha mafuta badala ya siku tisa na hivyo kuleta unafuu kwa mlaji na kupunguza gharama ambazo Serikali inalipa kutokana na muda wa meli kukaa bandarini.

Amesema kuwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ipo katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa sehemu maalum ya kupokea na kuhifadhi mafuta ijulikanayo kama single receiving terminal ambapo meli itakuwa na uwezo wa kupakua mafuta kati ya masaa 48 na 36 na hivyo kumaliza kabisa changamoto ya gharama za meli kukaa bandarini.

Amesema kuwa, kabla ya kuwepo taasisi ya PBPA upotevu wa mafuta kutoka bandarini ulikuwa ni asilimia 0.5 lakini hali ya upotevu kwa sasa imedhibitiwa na upotevu umepungua hadi asilimia 0.1.

Hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa upotevu kabisa kwa kufunga mita za kupimia mafuta (flow meter) pamoja na mfumo wa uangalizi wa flow meter (SCADA) ambao utakuwa chini ya PBPA na kwamba mfumo huu utakuwa unafanya kazi muda wote meli ikiwa inashusha mafuta na kuondoa upotevu wa mafuta kabisa wakati wa ushushaji wake.

Ameongeza kuwa, mfumo huo wa SCADA utaweza kuona shughuli ya ushushaji wa mafuta kwa bandari za mikoa inayopokea mafuta ambayo Tanga, Mtwara na Dar es Salaam.