Ataka huduma za kibiashara mgodini wazawa wapewe kipaumbele
Na Issa Mtuwa-WM, Geita
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amesema yapo mambo mengi yanayozungumzwa na kukubaliana kati ya Serikali na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) hususani ulipaji wa kodi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii (CSR), lakini bado baadhi hakubaliani nayo hususani suala la utekelezaji wa masuala ya utoaji huduma za kibiashara (Local Content), kwani nafasi hiyo ndio inayowapa wazawa kushiriki shughuli za uchumi kupitia Sekta ya Madini.
Hayo ameyasema mkoani Geita baada ya kuutembelea mgodi huo mkubwa wa Dhahabu wa Geita (GGML) ili kukagua shughuli zinazofanywa mgodini hapo.
Amesema, fursa za watu kushiriki katika utoaji huduma za kibiashara mgodini, ni muhimu kuwapa fursa wazawa ili kuinua uchumi wao na taifa.
Ameongeza kuwa, kazi zinazoweza kufanyika mgodini lazima zifanywe na Watanzania na kwamba kitendo cha hoja ya GGML kutaka kutoa huduma za kufanya tathmini za uingizaji umeme mgodini hapo, hawezi kuidhinisha, vinginevyo Wizara ya Nishati iseme hakuna mtaalam hapa nchini wa kufanya kazi hiyo.
Biteko amezungumzia pia, kuhusu haki ya wananchi hasa kwenye migogoro ya fidia. Aliongeza kuwa, hayupo tayari kuona hata mtu mmoja anadhulumiwa haki yake inayopitia sekta ya madini.
Anabainisha kuwa, kijiji cha Magema wananyanyasika kuhusu mahali wanapoishi, huku mgodi ukihitaji eneo hilo, toka walipoomba walipwe fidia mpaka leo na jambo hilo halijatekelezwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema, ameteua kamati ya wataalam mbalimbali kufuatilia na kuweka mpango mkakati utakaowahusisha wananchi katika kutoa huduma za kibiashara mgodini hapo kutoka asilimia 31 hadi asimilia 80, huku akiwa tayari kwenda Magema kufanya tathmini ya uhakiki nani mwenye haki na nani asie na haki ili utekelezaji wa fidia ufanyike.
Makamu wa Rais wa Mgodi wa GGML, Simon Shayo amesema, mgodi wao upo siku zote kushirikiana na kutekeleza maelekezo ya serikali. Kuhusu utekelezaji wa maagizo ya serikali kuhusu suala la umeme, Local Content na tathimini ya fidia yatazingatiwa.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati