November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodaboda wanavyokuwa changamoto kufifisha ndoto za wasichana

Na Penina Malundo

LICHA ya Serikali na taasisi mbalimbali ikiwemo ya Msichana Initiative kuanzisha programu mbalimbali za kuhakikisha wasichana wanakuwa katika misingi imara na kutambua thamani zao walizonazo bado baadhi yao wanakabiliana na changamoto mbalimbali.

Miongoni mwa changamoto kubwa inayowakumba wasichana wengi hususani waishio maeneo ya mbali na shule ni pamoja na madereva bodaboda kuwarubuni mabinti hao na kuwaingiza katika mitego ya kuwahusisha na masuala ya kingono.

Wanafunzi hao wamekuwa wanakabiliana na gadhabu hiyo hasa kipindi cha kutoka madarasa na kurudi nyumbani ndio muda pekee ambao madereva hao wanatumia mianya ya kuwarubuni mabinti wengi na kusababisha kukatisha ndoto zao wanazozisimamia . Madereva hao wamekuwa wanajipanga katika kukamilisha adhima hizo kwa kuwavizia barabarani kwa kuwa ujua muda ambao wanafunzi hao wanaotoka shuleni na kuanza kuwarubuni kwa kuwabeba bure.

Rosemary Muta sio jinalake halisi (15) anaesoma shule ya Msingi Kilomo iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani ,anasimulia mkasa anaokumbana nao njiani wakati akiwa anatoka shule na kurudi nyumbani anasema amekuwa anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo umbali wa kutoka nyumbani kwenda shule au kutoka shule kwenda nyumbani kukutana na vikwazo mbalimbali katikati(njiani ) kabla ya kurudi nyumbani au kufika shuleni.

Anasema changamoto za kurubuniwa na madereva bodaboda ni changamoto za kila siku ambazo wamekuwa wakikutana nazo,ambapo yeye tangu ameanza kidato cha kwanza mwaka huu ,katika shule hiyo hadi sasa amekuwa akipambana nazo.

”Tumekuwa tunakutana na changamoto hizi kila siku lakini tunakuwa tunazikataa,unakutana na mtu kila siku unamkuta katika eneo hilo wakati unatoka shule na ukifika katika eneo hilo anakuambia upande katika pikipiki yake,”anasema na kuendelea

”Kwa kuwa mimi najielewa na kujitambua najua nimefata nini shuleni najua anamaanisha nini uwezi kumuuliza kuwa anamaanisha nini kukusubiri kila siku,ila unapofika eneo hilo utamsikia akisema ”Panda unaweza kuja kuwa Rais wa baadae na kufanya vitu vingine sisi tukaja tukakuoa”anaongea maneno kwa mafumbo ambayo mtu hawezi kuelewa,”anasema.

Anasema muda mwingi wanasimamisha wakati wa kutoka darasani kurudi majumbani mwao ila kwa kuwa yeye anajitambua amekuwa hawezi kushawishika na maneno yao kwa kuwa sio mara moja wamekuwa wakiwasumbua.

*** Aishukuru Msichana Initiative kwa masomo ya Kujitambua Rosemary anasema Taasisi ya msichana Intiative chini ya Mradi wake wa One Girl Plus,umewasaidia kwa kiasi kikubwa hasa wao wanaotoka mbali na shule kwani wanakutana na changamoto nyingi ikiwemo ya lifti ambayo imekuwa ni hatari kwao.

Anasema kuzoea na madereva hao ni hatari kwani wanauwezo wa kukubadilisha ktabia na kuharibu ndoto zako kwa kukupa vishawishi ambavyo vinakuja kugeuka kuwa hatari katika maisha yao.

‘Nawashukuru sana katika kuja kunisaidia kuniongezea uelewa naamini nitazidi kufanya vizuri zaidi katika masomo yangu kwani kujiamini,kujitambua na kutimiza ndoto yako ni kitu muhimu sana katika umri wetu,”anasema na kuongeza

”Pia naishukuru taasisi hii kwa kuoa ni namna gani sisi wasichana tunapata vishawishi njiani na kuamua kuja na Baskeli ambazo wametupatia kuhakikisha tunatimiza ndoto zetu mimi nawashukuru sana kuona hili kwetu na tunawahidi kusoma kwa bidii ili tuje kutimiza ndoto zilizopo katika mioyo yetu,”anasema.

Kwa upande wake Careen Robson kutoka Shule hiyo kidato cha Tatu anaishukuru taasisi hiyo kuwasaidia kwa kuwapa elimu ya mambo mengi ambayo watoto wa kike wamekuwa wakikabiliana nayo.

Anasema ni watoto wa kike wachache ambao wanaweza kutambua ndoto zao hivyo ujio w taasisi hiyo kwao umekuwa na faida kubwa ya kuwapa fursa kubwa kujitambua na kujua thamani zao.

”Baadhi ya watu walikuwa hawana ndoto ila baada ya masomo haya imetufanya kuanza kuishi katika ndoto zetu na kuzipambania ndoto zetu,hii imetusaidia kujitambua malengo yangu na kupambana na vishawishi ninavyokutana navyo barabarani kutoka kwa madereva boda boda kuturubuni,”anasema na kuongeza

‘Miongoni mwa challenge kubwa wanayopitia sasa ni bodaboda kutoa lifti na kuanza kuleta mazoea ili mradi akupate, mimi ninavyoona hakuna mwanaume mwenye akili ambauye atahitaji Mwanamke asie soma kwa sisi hapa tunadanganywa tu ambapo wakitupa ujauzito ukimbia na kututerekeza,”anasema.

Mwalimu wa Malezi wa Shule Sekondari Kilomo,Magreth Tukay amekiri kuwa madereva boda boda wamekuwa wakiwachanganya sana watoto hao wakike hasa kwa waele watoto ambao makwao maisha yao ni duni na anatembea zaidi ya kilomita 4 kutoka kwenye lami kufika shuleni.

Anasema hali hiyo inawafanya wanafunzi kushawishika na kujikuta anadumbukia katika maisha ambayo sio yao kwa kumfata dereva huyo wa bodaboda ili aweze kumsaidia.

”Najitahidi sana kuwasimamia mabinti hawa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kama hii ya Msichana kwa kusimama na kuwaambia ukweli namna ya udanganyifu unaofanywa na watu hao katika kuharibu ndoto zao,”anasema.

Anasema ukishafundisha kujiamini na kujithamini kikubwa ni kuhakikisha mtu anatimiza ndoto zake ambapo kwa mwaka huu wameweza kubarikiwa kutokuwa na mwanafunzi hata mmoja akiwa mjamzito tangu mwaka 2019 hadi sasa.

Amesema programu ya watoto wa kike ya kujitambua angalau imekuwa inawasaidia kwa kiasi kikubwa kunusuru mabinti hayo kupata ujauzito kuanzia kidato cha kwanza hadi nne tofauti na miaka 2019 na 2018 ndipo shule hiyo ilikuwa ikikumbwa na wasichana kuwa wajawazito.

***Taasisi ya Msichana Initiative Yanena Furahini Michael Meneja miradi wa Taasisi ya Msichana Initiative anasema wamfika katika shule hiyo ya Kilomo kwaajili ya programu ya One Girl Plus ambayo ni prrogram iliyokusudia kutengeneza mazingira salama kwa watoto wa kike wa Sekondari.

Anasema watoto hao wakike wanajifunza masuala ya kujitambua,kujiamini na kuwa na ndoto kubwa kutumia mchezo wa kadi ambao unamaneno yaliyopo katika makundi matatu ikiwemo Kujitambua,Kujiamini na Ndoto kubwa .

”Kupitia kadi hizo watoto wa kike wanajifunza kupitia maeneo hayo matatu lengo ni kutengeneza wasichana wanaojitambua,kujiamini na kuwa na ndoto kubwa pamoja na kujua umuhimu wa elimu ili kupunguza mdondoke wa wanafunzi shuleni na kuongeza wanafunzi wengi zaidi wanaomaliza elimu ya msingi,”anasema.

Anasema programu kama hizo zimekuwa zikiwasaidia wanafunzi hao kujitambua na kuwaelekeza wanafunzi kuweza kupingana na vishawishi mbalimbali ambavyo wengi wao wanashindwa kumaliza shule na kutimiza ndoto zao.

“Programu hizi zinawafanya kujitambua wao ni wakinanani na kuwa na malengo kuepukana na vishawishi vya ndoa za utotoni,mimba za utotoni na kusababisha kuwepo kwa mdondoko shuleni wa wao kutotimiza ndoto zao walizojiwekea,”anasema

Akitoa wito kwa serikali na wadau wengine kuendelea kutengeneza programu hizio kwa sababu wanafunzi wanahitaji zaidi elimu ya stadi ya maisha kwani ni muhimu na inanafasi yake katika kusaidia kitu ambacho mwanafunzi anakipata darasani.

”Mradi huu wa One Girl Plus kwa awamu hii tumeamua kutembelea shule za Sekondari zilizopo Bagamoyo ikiwemo Shule ya Sekondari Kilomo na Nia njema ambapo tumewafikia wasichana zaidi ya 1000 katika shule hizo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na kuwapatia elimu ya kujitambua,kujithamini na kutimiza ndoto zao,”anasema.

*** Serikali yakemea vitendo hivyo Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike,Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima anasema wasichana wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi hivyo wanapaswa kutengenezewa mazingira rafiki ili kuweza kutimiza ndoto zao.

Anasema wapo watu wanaowabughudhi wasichana hao wadogo na kuwafanya kushindwa kutimiza ndoto zao kuacha mara moja tabia hizo kwani hatua kali dhidi yao zitaweza kuchukuliwa endapo wataripotiwa.

”wasichana msiogope kutoa taarifa kwa wale wanaowasumbua na kutaka kufifisha ndoto zenu,serikali inataka kutengeneza njia ambayo itakuwa rahisi kuripoti tabia za hao watu wanaowasumbua na kuwachukulia hatua stahiki,”anasema.

***Bodaboda anena Juma Hassan sio jinalake halisi Mkazi wa Bagamoyo mjini,anasema kuna baadhi ya madereva bodaboda ndio wanatabia ambazo sio nzuri badala ya kuwasaidia mabinti hao wao wanaruhusu hali ya kuwarubuni na kuwakatisha ndoto zao.

Anasema pia hali hiyo nayo inachanganywa na mabinti wenyewe nao kuwa sehemu ya madereva hao kuwataka kimahusiano kutokana na tamaa za kimwili kama vile pesa au simu za mkono hali inayofanyamadereva hao kuwarubuni.

”Kuna muda tukikaa katika vijiwe vyetu uwa tunapiga stori kama hizi kwanini mabinti wa shule wanakuaga wa kwanza kuonyesha hali ya kuwataka tunasema ni kwa sababu ya tamaa zao ambapo baadhi ya madereva wanasema wao wanawakubali ili mradi kukaa nao kwa muda wanapowahitaji ila uwa hawapo tayari kuwaoa kwa wakati huo,”anasema.

Naye Mmoja wa Wazazi wa wanafunzi wa Nia Njema Sekondari,Ramadhani Hassan anasema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia kundi la wasichana kujitambua na kujithamini kwani imekuwa na msaada mkubwa na kuleta matokeo makubwa kwa mabinti hasa katika kujitambua.

Anasema mbali na kutoa elimu pia wamekuwa na msaada mkubwa katika kutoa pikipiki ambazo zimekuwa msaada kwa watoto kuepukana na majanga mbalimbali ya njiani kama ubakaji na vishawishi vya njiani .

“Nashukuru kwa msaada wa baskeli kwa watoto wetu hawa kwani wamekuwa wkitembea umbali muda mrefu,kwa sasa hivi watatumia muda mchache wa kufika shuleni na kuwahi masomo yao,”anasema.