Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online, Dodoma
WAFANYABIASHARA wa vituo vya mafuta mkoani Dodoma wametakiwa kuendelea kutoa huduma kama kawaida kwa kuwa Mamlaka ya Udhibiiti Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) imeishafanya mazungumzo na wafanyabiashara kubwa ili kuwapatia nishati hiyo.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Mawasiliano na uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo wakati akizungumza na Majira leo mjini hapa kuhusiana na taarifa za kuwepo kwa mgomo wa wauzaji wa mafuta katika vituo 20.
Amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanaingia mikataba na wafanyabiashara wakubwa wanaowasambazia nishati hiyo hatua ambayo itasaidia kutoishiwa mafuta na bila kuvunja makubaliano baina yao.
Kaguo ametoa kauli hiyo wakati alipoulizwa na Mtandao wa TimesMajira kuhusiana na taarifa za kuwepo mgomo wa kuuza mafuta katika vituo ishirini jijini Dodoma.
Wakizungumza na TimesMajira Online leo madereva wa magari hayo wamesema kuwa kuna changamoto kubwa ya kupata mafuta katika mkoa mzima wa Dodoma, hivyo kujikuta wakilazimika kushindwa kutimiza majukumu yao.
“Tunasikitika sana kuona mji mzima hauna huduma ya mafuta, wengine tumeahirisha safari zetu kwa kukosa mafuta kila tukiwauliza wauzaji hatupati majibu sahii. Tunaomba Mamlaka zinazohusika kuingilia kati suala hili,” amesema Lister Peter.
Mmoja wa wamiliki wa Kituo cha Mafuta jijini hapa ambaye hakupenda jina lake kutajwa, amesema mgomo wao umetokana na wafanyabiashara wakubwa kukaidi maelekezo ya Serikali ya kuwataka kushusha bei ya mafuta tofauti na bei walizonunulia mafuta hayo, jambo ambalo ni hasara kwao.
Meneja wa Kituo cha Oil Com jijini hapa, Salum Awadhi, amesema kitendo cha wafanyabiashara kuficha mafuta kimepelekea hata wao kama wafanyabiashara wadogo kupata hasara, kwani wanapaswa kulipa wafanyakazi kupitia kuuza mafuta.
“Sisi hatuna tatizo hatufichi mafuta, bali yameisha kwenye tenki na sisi tunategemea wafanyabiashara wakubwa walioko Dar es Salaamu ili na sisi tuuze, hivyo tunaomba Serikali iingilie kati suala hili,” amesema Salumu.
Mwandishi wa habari hii alipomtafuta Kamishna wa Petroli na Gesi wa Wizara ya Nishati, Adamu Zuberi kuhusiana na mgomo wa wauza mafuta, amewataka wananchi kuwa na subira kwa hizi siku chache.
Amesema tayari serikali imewachukulia hatua wale wafanyabiashara wakubwa wa mafuta ambao walienda kinyume na leseni zao, ambapo wengine walikiri makosa yao.
“Niwaombe wananchi mtegemee mambo mazuri wafanyabiashara wengi wamekiri tatizo hilo Serikali ilikuwa imewafungia, hivyo iko kwenye utaratibu wa kuweka mambo mazuri ili wafanyabiashara wadogo waweze kufanya biashara zao, kwani takwimu zinaonesha mafuta yapo ya kutosha,” amesema Zuberi.
Hivi karibuni Waziri Dkt. Medard Kalemani alitoa siku saba kwa EWURA kuhakikisha wanawatafuta na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wakubwa wanaoficha mafuta ili baadaye waweze kuuza mafuta hayo kwa bei kubwa. Dkt. Kalemani alisema wamebaini mchezo unaofanywa na wafanyabishara wakubwa wa mafuta kutokana na bei iliypo sasa kuwa chini baada ya kushuka kwenye soko la dunia.
Amesema EWURA inatakiwa kuwasaka wafanyabiashara hao na kuwachukulia hatua kali ikiwemo ya kuwalipisha faini au kusitishia leseni zao za kuuza mafuta.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili