November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wahimizwa kutumia mfumo wa ‘Kilimo M’

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amewataka wakulima nchini kuutumia Mfumo mpya wa ‘Kilimo M ‘ wenye lengo la kukuza sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza mkoani Morogoro na wakuu wa vyuo vya mafunzo ya Kilimo 29 vilivyopo nchini Kusaya amesema kuwa, mfumo huo ambao ni wa mawasiliano ya simu baina ya mkulima na Ofisa Ugani kumpa fursa mkulima kupiga simu wakati wowote pindi anapokuwa na changamoto ya masuala ya kilimo.

Amesema wakulima wanapopiga simu wanapatiwa ufumbuzi muda huo huo badala ya kumsubiri Ofisa ugani mpaka afike shambani.

Wakuu wa vyuo mbalimbali wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya.

“Kwa hiyo sasa mnaona mahusiano yalivyorahisishwa kwa wakulima kupata ushauri wa kitaalam mara moja ,Serikali imefanya jitihada za kuhakikisha kilimo kinakuwa chenye tija na kumnufaisha mkulima,” amesema Kusaya.

Amesema, jitihada hizo pia ni pamoja na kuanzishwa kwa mpango wa maendeleo wa sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) ambao unalenga kubadili Kilimo na kukifanya kiwe cha kibiashara na kuinua uchumi wa mkulima.

Kwa mujibu wa Kusaya, amesema katika mpango huu wakuu wa vyuo ni wadau muhimu katika kuendesha na kusimamia mafunzo ili waweze kuzalisha maofisa ugani wenye weledi.

“Kama wakuu wa vyuo mtatumia mitaala inayoendana na wakati kutoa mafunzo ya masuala ya kilimo, hakika mtatoa mchango mkubwa na nchi itapata wagani wenye weledi na sekta ya Kilimo itaendelea kukua,”.

“Kunapokuwa na wagani wenye weledi, sekta ya kilimo itakua na kuchangia kwenye pato la Taifa kwa kiasi kikubwa kwani inachangia asilimia 28 ambapo sekta ndogo ya mazao pekee inachangia asilimia 16.2,” amesema kiongozi huyo.