November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi Ilemela wahimizwa kujenga tabia kupima hali zao za lishe

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wito umetolewa kwa watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani hapa kujenga tabia ya kupima hali zao za lishe ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, moyo, utapiamlo na mengineyo.

Wito huo umetolewa na Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Pili Kassim wakati wa zoezi la upimaji wa lishe lililoratibiwa na kitengo cha lishe cha halmashauri hiyo Agosti 21,lilioenda sambamba na upimaji wa shinikizo la damu kwa lengo la kujua hali za lishe za watumishi na kutoa elimu ya lishe bora kulingana na hali zao za lishe.

Ameeleza kuwa wameona kuna haja ya kupima hali ya lishe kwa watumishi kwani wengi wao hawana muda wa kufuatilia hali zao za lishe kutokana na majukumu mengi walionayo.

“Nawasisitiza watumishi kujenga tabia ya kupima hali zenu za lishe mara kwa mara angalau mara moja kwa mwezi, kuzingatia ulaji unaofaa pamoja na kufanya mazoezi kwa kufanya hivi kutaepusha magonjwa mbalimbali,”ameeleza Pili.

Pia ameeleza kuwa katika zoezi hilo takribani watumishi 60 walijitokeza kupima hali zao za lishe kati yao 20 wamekutwa na uzito uliokithiri wapo pia waliokutwa na hali nzuri ya lishe ambapo wote hao walipatiwa elimu ya namna nzuri ya ulaji wa vyakula.

Kwa mujibu wa Pili ameeleza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na halitaishia kwa watumishi wa makao makuu bali litafika hadi ngazi za mitaa ambapo kwa upande wa watumishi wa Makao Makuu zoezi litafanyika kila robo ya mwaka ambapo kwa upande wa watumishi waliopo ngazi ya kata zoezi litafanyika mara mbili kwa mwaka.

Ofisa Lishe Joyce Albert amesema upo umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa watumishi na wananchi kwa ujumla ili kuweza kuimarisha hali zao la lishe.

Ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa vipimo hivyo vya lishe watumishi wengi wamekutwa na uzito uliokithiri hivyo amewahimiza kujitokeza kupima hali zao za lishe pindi fursa kama hizi zinapojitokeza.

Kwa upande wao baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa nyakati tofauti wamepongeza zoezi hilo la upimaji wa hali ya lishe kwani wengi wao walikuwa hawana elimu ya kutosha juu ya lishe bora ambapo wameshauri kuwa zoezi hilo liwe endelevu kwa kuongeza na vipimo mbalimbali.

Chami David Sollo ni mtumishi wa Divisheni ya Utawala upande wa utunzaji wa kumbukumbu amesema kuwa, kupitia zoezi hilo ameweza kupata elimu juu ya namna bora ya kuzingatia ulaji wa vyakula na kufanya mazoezi kitendo ambacho kitawakinga dhidi ya magonjwa na kuomba zoezi hilo kuwa endelevu kwani lina manufaa kwa wengi

Joyce Kanuda Mwanafunzi wa Field amepongeza zoezi hilo na kusema kuwa hapo awali alikuwa akikabiliwa na ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya namna bora ya kuzuia unene usiofaa kwa afya yake sanjari na kujua juu ya namna bora ya kuzingatia makundi ya chakula hivyo kushukuru kwa elimu iliyotolewa huku akiwata watumishi wengine kutumia elimu iliyotolewa kwa ufasaha nyumbani mwao

Naye Rhoda Nyamsenda kutoka ofisi ya utunzaji wa kumbukumbu, amesema kuwa imekuwa kawaida yake kufika hospitali kwa ajili ya kupima afya yake na kusema kuwa amefurahia zoezi hilo kusogezwa eneo la kazi kwani imewarahisishia kuendelea na kazi sambamba na kujua hali zao za lishe.

Florence Vedasto kutoka Divisheni ya Maendeleo ya Jamii amesema ameamua kufika kupima kwa sababu alitaka kujua uzito wake na kulinganisha na urefu ambapo amejifunza namna ya ulaji wa watu wengi sio mzuri huku akishauri vipimo vingine viongezeke ili kuwezesha watumishi kujua hali zao za afya huku akiwahimiza wenzake kujitokeza kupima pale fursa kama hizo zinapojitokeza.

Juma Kingh’ola ni mtumishi wa Divisheni ya Miundombinu amesema amejifunza mengi ambayo alikuwa hayafahamu ikiwemo matumizi bora ya chakula kuweza kujikinga na uzito uliokithiri na magonjwa yasioambukizwa

“Ukizingatia matumizi bora ya lishe unaweza kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kama vile presha lakini si hivyo tu utajikinga na uzito uliokithiri,” amesema Juma.