November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA yawanufaisha Vijana 3,258 kukuza ajira na ujuzi kupita programu ya E4D

Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline,Dodoma.

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kupitia programu yake ya Kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo Afrika (E4D)imewanufaisha jumla ya vijana 3,258 kupata mafunzo ya ajira na ujuzi.

Jumla ya Vijana  3,258 wamenufaika na mafunzo katika Vituo vya veta vya Dodoma ,Manyara, Lindi,Singida Mikumi Gorowa na Dakawa  kupitia programu ya kukuza ajira na ujuzi Kwa maendeleo Afrika(E4D) ulioanza kutekelezwa mwezi mei mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Agosti 22 ,2023 ,Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu VETA,Abdallah Ngodu kuhusu ujio wa   Kongamano la ajira  litakalofanyika tarehe 24 mwezi huu katika Uwanja wa Nyerere Square jijini Dodoma lilobeba kauli mbiu isemayo  “Ufundi Stadi kwa Fursa zaidi za Ajira”

Ngodu ametaja taja vijana hao waliopata mafunzo ni kutoka katika vituo vya VETA vya Dodoma,Manyara ,Lindi,Singida,Mikumi Gorowa na Dakawa ambapo amesema idadi ya Vijana hao wanatarajiwa kuwa nguvukazi yenye ujuzi kutokana na mradi wa huo na itatumika katika kukuza ajira kwenye miradi ya kimkakati ya uwekezaji kama bomba la mafuta na Bwawa la Nyerere.

Amesema  kuwa utekelezaji wa Mradi wa E4D unahusisha ushiriki wa viwanda ambapo mpaka sasa viwanda/makampuni zaidi ya 20 yamethibitisha kushiriki na kuonesha huduma na bidhaa zao kupitia kongamano hilo.

“Tunaamini kuwa makampuni pia yatapata fursa muhimu ya kuthibitishiwa kwa uhalisia kuhusu umahiri na ujuzi wa wahitimu/wanufaika wa mafunzo ya ufundi stadi ili wajenge imani na hatimaye kuwapatia fursa za ajira vijana hao,” amesema Ngodu

Aidha amesema kuwa katika kongamano hilo kutakuwa na maonesho ambayo yamelenga kujenga uelewa juu ya fursa za ufundi stadi zilizopo kwenye Mradi, kukuza uwezo wa kuajirika (Kujiajiri/Kuajirika) kwa wahitimu/wanufaika wa kozi zinazotolewa na Vyuo vya VETA chini ya Mradi wa E4DT, Vilvile kupitia Kongamano hilo wanafunzi/wanufaika watakutanishwa na waajiri ili waweze kushirikishana kuhusu taarifa za soko la ajira. 

Pia wahitimu wataonesha umahiri wa ujuzi wao katika bidhaa walizotengeneza na miradi yao wanayotekeleza.

“Kupitia kongamano hili wananchi watapata fursa ya kujionea shughuli zinazofanywa na wahitimu/wanufaika wa mradi wa E4DT pamoja na kupata taarifa juu ya fursa za mafunzo ya ufundi stadi zinazopatikana kwenye vyuo vya VETA nchini,”amesema Ngodu.

Amesema kuwa wakati wa Kongamano hilo, kutakuwa na uwepo wa Taasisi za Fedha ambazo zitatoa fursa za uwezeshwaji hususan mikopo zinazoweza kuwanufaisha vijana waliopata ujuzi ili wawe na mitaji ya kuendesha shughuli za uzalishaji na kuongeza vipato na ajira endelevu.

Ngodu amefafanua kuwa  Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za Afrika zinazotekeleza mradi wa Stadi za Ajira kwa Maendeleo Afrika (E4D) unaofadhiliwa na Wizara ya Shirikisho la Ujerumani la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ) na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Korea (KOICA). 

“Mradi wa E4DT ulianza kutekelezwa mwezi Mei, 2022, ukilenga kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana 4000 nchini, katika fani za Ufundi Bomba wa majumbani (Domestic Plumbing), Ufundi Bomba Viwandani (Industrial Plumbing), Ufundi wa Uchomeleaji Vyuma Viwandani (Industrial Welding) na Ufundi wa Mekatroniki (Mechatronic),”amesema Ngodu.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo Cha ufundi Cha  Veta Dodoma Stanslaus Ntibara amesema hadi kufikia tarehe 19 mwezi huu  jumla ya wanafunzi  1806  wa Mkoa wa Dodoma walikuwa wameshahitimu mafunzo hayo.

Naye Mwakilishi Mshauri wa program kutoka Shirika la GOPA,  Leah Dotto amesema mradi huo  unalenga kuwaandaa vijana kupata ajira kwenye uwekezaji ambao unafanyika hapa nchini na kuweza kujiajiri .