Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Mbeya
SIKU chache tangu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi, kutoa maelekezo ya kuharakisha ujenzi wa barabara jijini Mbeya, kazi hiyo imeanza kushika kasi huku maeneo yaliyokuwa na changamoto ya upitaji yakifunguliwa ili kurahisisha shughuli za wananchi.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa maelekezo hayo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga amesema, wameendelea kufungua njia zinazotumiwa na wananchi ili kupunguza adha iliyokuwepo kutokana na ujenzi wa barabara hiyo.

Amesema eneo la Kabwe ni miongoni mwa maeneo yanayotekelezwa katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Sadaka kuelekea Physical 29, ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha wananchi wanapata njia za kupita wakati ujenzi ukiendelea.
“Tumetambua jumla ya maeneo 116 kuanzia Msagala hadi Fisi ambayo yalihitaji kufunguliwa ili wananchi waweze kupita. Maeneo hayo tumeshayafungua na sasa tunaendelea kuyaboresha ili yaweze kupitika bila shida,”amesema Bishanga.
Ameongeza mkandarasi ameagizwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kasi na kwa ubora unaotakiwa, huku hatua za kuweka saruji zikiendelea katika maeneo husika, lengo ni kukamilisha mradi bila kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Patrick Mwalunenge amesema,ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo baada ya kutembelea maeneo ya mradi na kujionea kazi zinazoendelea chini ya usimamizi wa TANROADS na mkandarasi.
Amesema kasi hiyo imeongezeka na njia zinazopitiwa na wafanyabiashara na wasafirishaji zimeanza kufunguliwa, akitolea mfano eneo la Mdope ambako vifusi vimewekwa ili kurahisisha magari kuingia na kutoka katika maeneo ya biashara.
Pia amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa Mbeya Mjini, ikiwamo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuongeza shughuli za biashara na kuboresha mwonekano wa jiji.
Amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali ambapo ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuboresha miundombinu huku akiwashauri wasimamizi wa mradi kuhakikisha maeneo ya biashara yanaendelea kufikika wakati ujenzi ukiendelea na kwamba sehemu ambazo bado hazijawekewa lami zimwagiwe maji ili kupunguza vumbi linaloweza kuathiri wafanyabiashara na wananchi wanaotumia barabara hizo.
Akizungumzia hali ilivyokuwa kabla ya kutolewa kwa maelekezo ya Makamu wa Rais, mmoja wa wananchi wa Jiji la Mbeya Amos John amesema,kulikuwa na changamoto ya kupita katika baadhi ya njia za mitaa, hali iliyosababisha bajaji, bodaboda na magari kupata shida kufika katika maeneo mbalimbali.
Amesema baada ya maelekezo hayo, njia zimeanza kufunguliwa na kuwekwa vifusi, hatua ambayo imerahisisha usafirishaji na kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaotumia barabara hizo.
Naye mwananchi mwingine anayefanya shughuli zake katika eneo la Mdope, karibu na vibao vya Shule ya Rwanda Nzovwe Emanuel Mwakalinga amesema ameshuhudia maendeleo ya ujenzi huo kwa kasi kubwa, akieleza kuwa kuwekwa kwa vifusi kumeboresha upitaji wa magari na kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya biashara.
Alisema pia hatua zilizochukuliwa katika kufungua njia za kuunganisha mitaa na barabara kuu zimeanza kusaidia wananchi waliokuwa wakipata shida kufika katika maeneo yao ya shughuli za kiuchumi huku wanatarajia barabara hiyo itakapokamilika itarahisisha usafiri, kuchochea biashara na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi jijini Mbeya.


More Stories
Mchengerwa: Hakuna Mtanzania atakayekosa matibabu
Dkt.Homera akutana na Watendaji wa Kampuni ya Vivo Energy
TCB, MAKAZI SOLUTIONS watanua fursa za umiliki wa viwanja