Na Penina Malundo,TimesMajira
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limeipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanza kusajili wananchi wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi kwenye Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, likisema hatua hiyo itasaidia kupanua upatikanaji wa huduma za afya nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Mtwara, Mkurugenzi Mkazi wa WHO nchini Tanzania, Dkt. Alex Ntale Ga, amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma bora za afya bila kukabiliwa na changamoto za kifedha zinazotokana na gharama za matibabu.
Amesema ushirikishwaji wa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na mfumo wa bima ya afya.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya nchini kupitia uimarishaji wa miundombinu, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Amesema maboresho hayo ni muhimu katika kuhakikisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote unatoa huduma bora na kwa ufanisi, kulingana na mahitaji ya wananchi.
Uzinduzi wa awamu ya pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote uliofanyika mkoani Mtwara ulienda sambamba na uzinduzi katika mikoa mingine tisa, ambayo ni Mwanza, Mbeya, Arusha, Kigoma, Dodoma, Shinyanga, Tanga, Songwe na Simiyu.

Uzinduzi huo wa pamoja unaashiria ushirikiano wa kitaifa katika juhudi za kupanua huduma za bima ya afya na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za matibabu.


More Stories
Mchengerwa: Hakuna Mtanzania atakayekosa matibabu
Maagizo ya Makamu wa Rais yaanza kutekelezwa
Dkt.Homera akutana na Watendaji wa Kampuni ya Vivo Energy