Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Nsimbo
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeunda kamati maalumu ya kupitia mipaka ya hifadhi ambapo itawasilisha taarifa ya mipaka ya mapori yote na kutangazwa kwenye gazeti la serikali.
Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),Mabula Misungwi Nyanda amebainisha hayo Agosti 14,2023 wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoa wa Katavi ambapo amefanya kikao cha ndani na viongozi wa wilaya pamoja na vikao vya nje na wafugaji nyuki wa Kata ya Nsimbo na Ugalla.
Nyanda amesema kuwa wakati wa kuwekwa kwa alama za mipaka ya mapori,wananchi watashirikishwa lakini kwa sasa wanapaswa kuzingatia mipaka iliyopo.
Kamishina huyo amesema kuwa mkanganyiko wa mipaka ya uhifadhi za taifa,mapori ya akiba na misitu inatokana na mabadiliko ya kiuhifadhi ambapo baadhi hayakuwepo kwa mfano Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla kwa sasa hawaruhusu matumizi yoyote ikiwa hapo awali ilikuwa sehemu ya pori la akiba.
“Mabadiliko hayo bado serikali inayafanyia kazi kwa ngazi ya Wizara kwa sababu TAWA nao hawaanzishi maeneo na kuweka mipaka yao tu,utaratibu uliopo wa kutenga maeneo kwa upande wa hifadhi wa wanyamapori ni Wizara ambayo ina mamlaka kupitia idara ya wanyamapori kutenga maeneo hayo aidha yawe ya hifadhi ya taifa,pori tengefu au pori la akiba,” amesema Nyanda.
Amesema mkanganyiko wa mipaka unatokana na wananchi kushindwa kuelewa pori la akiba,misitu na hifadhi ya taifa inaishia wapi na nani anayehusika na taratibu zake zikoje ambapo suala hilo linapaswa kueleweka kwao kwa ajili ya kuzuia migogoro na kwa kuzingatia hilo amewaelekeza watendaji wa TAWA kutoa elimu.
“Wananchi wanatakiwa kuelewa mapori maana yake ni nini na pori lipi na linahusika na nini na lipi halihusiki na nini hii itawasaidia wajue wafanye nini na waishije kuendesha maisha yao kwani kutokufahamu ni sawa na kutembea gizani,”amesisitiza.
Aidha Kamishina huyo amesema kuwa kuna pengo la kutokufahamiana kati ya watendaji wa TAWA na wananchi jambo ambalo linasababisha migongano isiyokuwa ya lazima kwa kuwa na dhana potofu ya kila mtu dhidi ya mwenzake.
Hata hivyo ametoa wito kwa watendaji wote wa TAWA nchini kuliondoa pengo hilo kwani wananchi ni sehemu ya familia zao na majukumu ambayo wamepewa na serikali yasiwatenge bali wanapaswa kuwa na tahadhari na kila kitu kwa ajili ya maisha ya kesho.
“kwahiyo mimi na wasihi watendaji wenzagu tuliondoe hili pengo kama ni suala la elimu litolewe,”amesema Kamishina huyo.
Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Mkoa wa Katavi Anna Lupembe amemshukuru Kamishina huyo kwa kusikiliza kero za wafugaji wa nyuki na kuruhusu kusogezwa huduma ya upatikanaji wa vibali vya kuingia porini ambapo wananchi hulazimika kusafiri umbali wa Km 125 kwenda mji wa Inyonga Wilaya ya Mlele.
Lupembe amesema kuwa suala la wananchi kusafiri umbali mrefu ni kikwazo kwa juhudi za wafugaji nyuki kupiga hatua za maendeleo hivyo uamuzi wa vibali kutolewa katika Wilaya ya Mpanda ni wakumkoamboa mfuga hata mdogo wa nyuki.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa wananchi wa Jimbo la Nsimbo hawapendi kufanya uadui na Askari wa TAWA kwani kufanya hivyo ni kufifisha juhudi za kujikomboa kiuchumi kwao bali wanahitaji kupewa elimu.
Papi Mlela,awali akisoma risala ya mbele ya Kamishina Mkuu wa TAWA ametoa ombi kwake kupunguza gharama ya vibali vya kuingia ndani ya pori kwani ni kubwa ambazo wanashinda kuzimudu.
Vilevile wameomba kuruhusiwa kutumia usafiri wa pikipiki kwenda ndani ya pori kubebea asali ambayo wamekwisha kulina kwani itawafanya kubeba kwa wingi zaidi.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa