November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri William Lukuvi

Lukuvi aagiza wasajili wasaidizi hati za ardhi kutoa elimu kwa umma

Na Mwandishi Wetu, Singida

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka Wasajili WasaidIzi wa Hati kwenye Ofisi za Ardhi za Mikoa kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na faida ya ofisi ya Msajili wa Hati.

Akizungumza wakati wa kuzindua ofisi ya ardhi ya mkoa wa Singida jana Lukuvi amesema ofisi ya Msajili wa Hati ina jumla ya mihuri 34 yenye kazi mbalimbali ambazo Msajili Msaidizi wa Hati anaitumia kutekeleza majukumu yake.

Amesema, ofisi hiyo mbali na kutoa hati za ardhi lakini pia inasajili nyaraka mbalimbali kama vile uhamisho wa miliki, rehani na ubadilishaji jina ambapo wananchi wakipata elimu kuhusiana na faida zinazopatikana katika ofisi ya Msajili wa hati wataweza kuitumia vyema ofisi hiyo.

Amewataka wasajili wasaidizi wa hati kwenye ofisi za ardhi za mikoa kuhakikisha wanatoa elimu kuhusiana na ofisi zao kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo redio zilizopo katika mikoa yao kwa kuwaeleza wananchi huduma zinazotolewa kupitia ofisi zao.

“Msajili wa Hati amepewa mamlaka ya kurekebisha nyaraka mbalimbali, ni vizuri mkajitambulisha kwa wananchi ili watambue na kujua faida ya ofisi zenu kwani wakati mwingine wananchi wanagomabana mahakamani kwa kutosajiliwa nyaraka zao,” amesema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na ofisi ya msajili kuwa na faida katika kutoa hati za ardhi na kusajili nyaraka mbalimbali lakini pia ofisi hiyo inaiingizia serikali mapato yatokanayo na kazi zinazofanywa na ofisi hiyo.

Akielezea uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa Waziri Lukuvi amesema, pamoja na ofisi hizo kupelekewa wataalamu wa fani mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha utoaji huduma za ardhi lakini ofisi za ardhi za mikoa zimepatiwa vifaa mbalimbali vya upimaji kwa lengo la kuwezesha maeneo mengi kupimwa.

“Halmashauri kama hazina vifaa, badala ya kwenda kukodi vifaa vya upimaji kwa gharama kubwa kwenye makampuni ziende kukodi ofisi za ardhi za mikoa ili kuwezesha zoezi la upimaji,” amesema Lukuvi.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa mkoa wa Singida ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili ameelezea uamuzi wa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa kuwa ni ufumbuzi wa matatizo ya ardhi kwenye mkoa wa Singida ambapo hapo awali kulikuwa na urasimu kutoka kwa watumishi wa sekta hiyo. Hata hivyo amesema ofisi hizo za ardhi za mikoa zitawawezesha wananchi kupata huduma za ardhi kwa wakati tofauti na huko nyuma.