November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DAWASA kutumia bilioni 425.9 kutekeleza miradi saba ya kimkakati

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imejipanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 425.9 kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi kupitia miradi ya kimkakati saba ikiwemo ya ujenzi wa bwawa la Kidunda,ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji pamoja na Kwala.

Hayo yalibainishwa jijini hapa leo,Agosti 11 ,2023 na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA,Kiula Kingu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na mwelekeo wa shughuli za mamlaka hiyo ambapo ametaja miradi mingine ya kimkakati ni mradi wa maji Mji wa Pangani Kibaha, ujenzi wa mradi kutoka Kimbiji-Kigamboni hadi jirani na Chuo cha Uhasibu (TIA), ujenzi wa mradi wa maji Kusini mwa Jiji la Dar es salaam na mradi wa uchimbaji visima virefu tisa eneo la Kigamboni.

“Miradi hii itakayotekelezwa inalenga katika kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa yale ya pembezoni,”amesema Kingu.

Kingu ameeleza kuwa pamoja na kuwekeza nguvu katika utoaji wa huduma za majisafi, DAWASA imejipanga kikamilifu na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira kupitia miradi mikubwa na midogo.

“Hii ni kwa sababu upatikanaji wa maji unapoongezeka unapaswa uambatane na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira,

“Katika Wilaya ya Kinondoni na Ilala, miradi ya kuchakata majitaka itajengwa katika maeneo ya Mbezi Beach na Buguruni, Mradi wa Mbezi Beach unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia ambapo jumla ya shilingi bilioni 132.3 zitatumika kujenga mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuchakata lita milioni 16 kwa siku,”amesema.

Ametaja mradi mwingine kuwa ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika ambapo katika awamu hii ni Mbezi beach, Kilongamwima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala na utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.

Aidha ameeleza kuwa DAWASA imekuja na ubunifu wa kujenga mifumo na mitambo midogo midogo ya kuchakata majitaka inayojengwa maeneo ya pembezoni ambapo zaidi ya lita 780,000 za majitaka zitakuwa zikichakatwa kwa siku.

“Miradi hii itajumuisha ujenzi wa vyoo vya umma 30 ambavyo vitasaidia kuboresha usafi wa mazingira,
miradi hii itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu na maeneo wanayoishi,

“Wakandarasi wanaotekeleza miradi wanaendelea na ujenzi gharama za miradi hii ni jumla ya shilingi bilioni 25.7 na wanufaika wa miradi hii wanakadiriwa kufikia milioni 1.8,”amesema Kingu.

Pia amesema Miradi hiyo ni ya kisasa na katika mfumo wake wa uchakataji majitaka itatoa gesi asilia kwa ajili ya kupikia, itatoa mbolea itakayoweza kutumika katika kustawisha bustani za miti na majani pia maji yatakayochakatwa yataweza kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, usafishaji wa barabara na mitaro ama kupoozea mitambo.