Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki ameliomba Shirika la World Vision Tanzania kuendelea kutoa huduma za kijamii na kiuchumi, kwani Tanzania bado inahitaji wahisani kama wao ili kuimarisha huduma za jamii.
Ameyasema hayo Julai 6, 2023 mara baada ya kufungua majengo ya shule ya Msingi Mnyuzi, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ikiwemo vyumba vya madarasa na nyumba za walimu yaliyojengwa na World Vision AP ya Mnyuzi.
“Tunawashukuru Shirika la World Vision kwa kujenga miradi yenye thamani ya bilioni 1.1,miradi hii itanufaisha wananchi zaidi ya 13,000,nakiri kuwa shirika hili mmekuwa mkifanya kazi katika mikoa zaidi ya 16 hapa nchini na huko kote mmeisaidia jamii kupata huduma bora ikiwemo elimu, afya, maji na shughuli za kiuchumi,”amesema Kairuki na kuongeza kuwa
“Ombi langu, na ombi letu kama Serikali, msisite kushirikiana na serikali kuwekeza kwenye miradi mingine, Tanzania bado tuna kizazi kichanga ambacho kinatakiwa kusaidiwa,bado tunahitaji huduma za afya na elimu,asilimia kubwa ya Watanzania bado ni vijana, na wanatakiwa kusaidiwa, hivyo, tunaomba mfike maeneo mengi zaidi ili wananchi wafaidike,”.
Kairuki amesema World Vision imefanya kazi nzuri sana kwenye Mkoa wa Tanga kwenye Wilaya za Korogwe, Handeni, Kilindi na Mkinga, hivyo anaamini shirika hilo litaendelea kufanya vizuri kwenye maeneo mengine ya Tanzania na kuweza kuisaidia Serikali kutoa hufuma za jamii.
Kairuki amewataka viongozi kuendelea kuwahudumia wananchi, kwani Serikali inapeleka fedha nyingi za maendeleo kwenye ngazi za wilaya, halmashauri, kata na vijiji, hivyo ni wajibu wa viongozi kuona zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kairuki amesema ili kuleta ufanisi kwenye Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), amesema watarudisha mameneja wa TARURA kuwa kila halmashauri badala ya wilaya. Nia ni kukuza ufanisi katika kutengeneza barabara za vijijini.
Awali, Mkurugenzi wa World Vision Tanzania Dkt. Joseph Mayala amesema miradi ilitotekelezwa kwenye Kata za Kwagunda na Mnyuzi ina thamani ya zaidi ya bilioni 1.1 na yote kwa ujumla wake inanufaisha jumla ya wananchi zaidi ya 13,700 kwenye kata hizo wakiwemo watoto.
Dkt. Mayala amesema kwenye shule ya msingi Mnyuzi kumejengwa vyumba vinane (8) vya madarasa kwa gharama ya zaidi ya milioni 264.1,ujenzi wa ofisi ya walimu gharama ya zaidi milioni 5.4, ujenzi wa vyoo katika shule ya msingi hiyo, Mseko na Lwengera Estate kwa gharama ya zaidi ya milioni 190 na ununuzi wa madawati 300 yenye thamani ya milioni 33.6, na ujenzi wa nyumba ya watumishi (2 in 1) katika shule ya msingi Mnyuzi yenye thamani ya zaidi ya milioni 99.
Wilaya ya Korogwe shirika la World Vision limefanya kazi kwa karibu na Serikali katika kutekeleza program za maendeleo maeneo mbalimbali tangu miaka ya 1990. Kati ya maeneo ambapo shirika limetekeza program za miaka 15 na zikamaliza muda wake ni pamoja na Mombo, Bungu na Magoma kwa sasa shirika linatekeleza program ya maendeleo ijulikanayo kama Mnyuzi AP.
Amesema eneo la mradi ni kata za Kwagunda, Mnyuzi na Hale katika vijiji 12 ambavyo ni Ubiri, Mng’aza, Mkokola, Magunga cheki, Kwagunda, Gereza East, Mkwakwani, Kwamzindawa, Mnyuzi, Lusanga, Ngomeni na Shamba kapori.
“Program ya maendeleo Mnyuzi inatekelezwa kwa ufadhili wa World Vision Hong Kong ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 2014 na inatarajiwa kufikia ukomo mwaka 2028 inayotekelezwa katika eneo hilo inalenga maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii, hususani watoto,”amesema Dkt. Mayala.
Miradi mingine ni ujenzi miundombinu ya kunawia mikono (10 tapes) na mfumo wa maji katika shule ya sekondari Mnyuzi yenye thamani ya zaidi ya milioni 14,ujenzi wa miundombinu ya kunawia mikono (10 tapes) na mfumo wa maji katika shule ya msingi Mng’aza yenye thamani ya zaidi ya 14.1,ujenzi wa miundombinu ya kunawia mikono (4 tapes) na mfumo wa maji katika Zahanati ya Mnyuzi yenye gharama ya zaidi ya milioni 5.
Ujenzi wa jengo la RCH na OPD katika zahanati ya Mnyuzi inayogharimu zaidi ya milioni 142, ujenzi wa nyumba ya watumishi (2 in 1) katika zahanati ya Mnyuzi unaogharimu kiasi cha zaidi ya milioni 91, ujenzi wa kichomea taka ( Incenerator) na Plancenta Pit katika zahanati ya Mnyuzi yenye thamani ya zaidi ya milioni 13, ujenzi wa choo (matundu 4) katika zahanati ya Mnyuzi yenye thamani ya zaidi ya milioni 22, ujenzi wa kichomea taka ( Incenerator) katika zahanati ya Magazini thamani ya milioni 9.5.
Ujenzi wa wodi ya kujifungulia (Delivery and Maternity) katika zahanati ya Magazini wenye thamani ya zaidi ya milioni 64, ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya milioni 18 pamoja na ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Mng’aza wenye thamani ya milioni 145.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa