Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Shinyanga
KAMATI ya Maendeleo ya Kata ya Mjini (WDC) Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa halmashauri hiyo ndani ya Kata hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa WDC Kata ya mjini Shinyanga,Diwani wa kata hiyo Gulam Hafiz Mukadam baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hiyo.
Gulam amesema wameridhishwa kuona jinsi utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata yake unavyotekelezwa kwa kuzingatia Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 na kwamba moja ya mradi mkubwa wa kimkakati ambao wameutembelea ni ukarabati wa soko kuu la Shinyanga Mjini.
“Kwa niaba ya wajumbe wangu wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Mjini, nichukue fursa hii kuwapongeza watendaji wetu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya chini ya Mkurugenzi wetu Jomaary Satura kwa kweli wametuboreshea Mji wa Shinyanga,”amesema na kuongeza kuwa
“Japokuwa sasa hivi Satura anahamishwa kwenye Manispaa yetu, lakini tunamshukuru sana kwa kutufanyia mambo makubwa katika mji wetu, ametupa ushirikiano wa kutosha na kutubadilishia mji huu wa Shinyanga, tutaendelea kumkumbuka wakati wote na kumuenzi kwa kazi nzuri alizozifanya,” ameeleza Gulam.
Diwani huyo ameitaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye kata yake pamoja na ile inayoendelea kutekelezwa hivi sasa kuwa ni pamoja na ukarabati mkubwa wa soko kuu la mjini Shinyanga ambalo kazi yake bado inaendelea ikitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu ambalo kwa hivi sasa litakuwa na ghorofa awamu ya kwanza ikiwa na vyumba zaidi 100.
Pia ujenzi wa maeneo ya kupumzikia watubkatika eneo la Phantom (mataa) na Kalogho ambapo hivi sasa wananchi wamepata sehemu nzuri za kupumzikia nyakati za mchana na hata usiku huku baadhi yao wakiendesha biashara ndogondogo za vyakula na vinywaji.
Ujenzi wa soko la machinga eneo la ofisi za CCM Shinyanga Mjini ambalo ujenzi wake umekamilika na hivi sasa linatumiwa na wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakiuza biashara zao mitaani na kandokando ya barabara na eneo maarufu la mtaa wa sukari.
Kwa upande wa sekta ya elimu Gulam amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha shule ya msingi Mwenge kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na matundu matatu ya vyoo hali ambayo amesema itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya mrundikano wa wanafunzi darasani.
Shule ya msingi Mwenge ni moja ya shule kongwe katika Manispaa ya Shinyanga ambayo ilifunguliwa rasmi mnamo mwaka 1938 na kwa sasa ina idadi kubwa ya wanafunzi huku vyumba vya madarasa vikiwa ni 19, madawati 600, viti 33 na meza 15 ambapo darasa moja linatumiwa na wanafunzi zaidi ya 100.
Kutokana na hali hiyo Diwani Gulam ametoa ahadi ya kutafuta wafadhili mbalimbali ili waweze kuisaidia shule hiyo ambayo viongozi na watu wengine maarufu hapa nchini akiwemo yeye mwenyewe wamesomea hapo ambapo ameshauri kuangalia uwezekano wa kujenga majengo ya ghorofa kutokana na uhaba wa eneo.
Katika taarifa yake, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mjini, Mathias Masalu amesema mbali na miradi ya maendeleo inayotekelezwa pia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Shinyanga wametatua changamoto ya uchakavu wa mtaro mkubwa wa maji ambao ulisababisha kero nyakati za masika kutokana na maji kujaa kwenye makazi ya watu.
Baadhi ya vijana wanaoendesha pikipiki za magurudumu matatu bajaji na zile za bodaboda za kusafirisha abiria mjini Shinyanga pia wameshukuru ujenzi wa maeneo ya kupumzikia katika mji wao ambapo pia bustani hizo zimetengewa maeneo ya maegesho ya bajaji na pikipiki zao.
“Kwa kweli tunawashukuru wenzetu wa Manispaa ya Shinyanga, chini ya Mkurugenzi Jomaary Satura kwa kazi nzuri ya uboreshaji wa mji wetu sambamba na kutukumbuka sisi waendesha pikipiki na bajaji za kusafirisha abiria kwa hivi sasa tuna maeneo mazuri ya kusubiria wateja wetu,”
“Mkurugenzi Satura pamoja na kwamba Rais Samia kaamua kumuhamisha kwa kweli alikuwa na maono ya hali ya juu ya kutuboreshea mji wetu, laiti Rais angetuuliza kwanza sisi wananchi wa Shinyanga tungemuomba amuache mpaka pale atakapokuwa ametimiza ndoto zake za kuuboresha mji huu wa Shinyanga,” ameeleza Jeilani Ramadhani.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa