Judith Ferdinand, Timesmajira online, Mwanza
Serikali na wadau mbalimbali nchini wameombwa kuhakikisha taulo za kike zinapatikana kwa urahisi, miundombinu ya kujihifadhia inakuwepo pamoja na maji safi na salama.
Ili kuwafanya mabinti na wanafunzi wa kike wanakuwa na hedhi salama wawapo shuleni na nyumbani hivyo kutimiza ndoto zao kama wanafunzi kiume na vijana.
Akizungumza na Timesmajira online,mmoja wa wanafunzi wa shule iliopo jijini Mwanza Irene Shelesta, ameeleza kuwa suala la hedhi salama kwa mabinti limekuwa changamoto kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kujihifadhia na kuhifadhia taulo zilizotumika shuleni hata nyumbani.
Irene ameeleza kuwa changamoto nyingine shule nyingi na maeneo mengi ya vijijini na pembezoni mwa miji kukosa maji salama ambayo ni muhimu wakati wa hedhi ambapo wa binti hutumia kujisafishia na kufanya kuwa na hedhi salama bila maambukizi yoyote.
Huku akisisitiza kuwa suala la hupatikanaji wa taulo za kike limekuwa changamoto kwa mabinti wawapo shuleni hata nyumbani kwani siyo wote wanaweza kumudu gharama.
“Unakuta shule kuna miundombinu ya kutupia taulo za kike zilizotumika lakini hakuna maji safi kwa ajili ya kujisafishia wala chumba cha kujihifadhia chenye usiri hivyo inakuwa changamoto sana kwetu,mfano wanaosoma shule za bweni ukikuta anatumia taulo za kike za kufua alafu maji hamna inakuwa ni changamoto hivyo wadau na serikali itusaidia kuweka mazingira rafiki ya kuwa na hedhi salama,”ameeleza Irene.
Akizungumza na Timesmajira online kwa njia ya simu Ofisa Maendeleo ya Mtoto,Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza (MYCN),Nuru Massanja, ameeleza kuwa suala la hedhi salama siyo la watoto wa kike na wanawake tu ni la kila mmoja serikali na jamii nzima katika kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa salama pale anapokuwa katika hedhi.
Hivyo serikali ihakikishe watoto wa kike wanapata maji salama wawapo shule kwa ajili ya kujisafishia pia hata nyumbani kuwe na upatikanaji rahisi wa maji kwa serikali kusogeza huduma karibu maana kuna kutumia taulo za kike za kufua ambazo zinahitaji maji ya kutosha kwa ajili ya kuzifua kwa matumizi ya baadae.
Pia kuhakikisha kuna kuwa na vyoo au vyumba vya kujihifadhia wakati wa hedhi wawapo shuleni vyenye usiri ambavyo mtoto wa kike atakuwa uhuru kubadilisha taulo za kike bila mtu yoyote kufahamu kama yupo hedhini.
Aidha kuwezesha miundombinu ya kuhifadhia taulo za kike zilizotumika shuleni mara atakapobadili kwa maana ya vichomea taka ili kumfanya binti kuwa na amani awapo shuleni.
“Serikali iangalie miundombinu ya kutupa taka yani taulo za kike zilizotumika ili baada ya kujisafishia anatupa uchafu kwenye mazingira mazuri kuliko kuweka kwenye begi na kusubilia mpaka atoke shule akatupe nyumbani,mwingine hawezi kufanya hivyo anaona aibu na kuona bora abaki nyumbani mpaka siku zake za hedhi zitakapoisha ndio aende shule wakati huo anakuwa amepitwa na masomo,” ameeleza Nuru.
Akizungumzia suala la upatikanaji wa taulo
za kike Nuru ameeleza kuwa serikali ina nguvu kubwa katika kuzingatia bei kwani siyo kila mzazi ana uwezo wa kununua taulo za kike kila mwezi kwa ajili ya binti yake hususani vijijini hivyo itoe bei elekezi kwa wafanya biashara ambayo itaendana na uchumi wa Watanzania walio wengi pamoja na kuhakikisha maeneo ya shule kwa kushirikiana na wadau zinapatikana wakati wote bure.
“Serikali waweke utaratibu wa kuhakikisha watoto wa kike shuleni kwa kila shule wanapata taulo za kike ambazo watatumia wawapo shuleni wakati wa hedhi ili wasishindwe kuhudhuria masomo kwa siku wanazokuwa hedhini,hata kama mzazi wake hana fedha ya kununua taulo za kike anajua akifika shule atazikuta hivyo kuendelea kusoma katika mazingira salama yanayoendana na hedhi salama,”ameeleza Nuru.
Sanjari na hayo Nuru ametumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuzungumza na watoto wao siyo wa kike tu bali wote kuhusu hedhi salama ili kuleta urahisi kwa mtoto wa kike kuwa katika mazingira rafiki.
“Kuwaelimisha watoto wote siyo wa kike pekee kwani uwezi jua atakayemsaidia binti anapokuwa katika hedhi kwenye mazingira ya shule au nyumbani kwani mtoto wa kiume akiwa anajua masuala kama hayo itasaidia kuwa na mazingira mazuri kwa mtoto wa kike wakati wa hedhi,pia elimu ya hedhi salama itawasaidia watoto kutojiingiza katika masuala ya mapenzi kwani anatambua kuwa muda gani anaweza kupata mabadiliko kwenye mwili na namna gani ya kujizuia,”ameeleza Nuru.
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Nyamanoro Lydia Hugo, ameeleza kuwa kukua kwa teknolojia kila siku vitu vinabadilika hata vya kujihifadhia wakati wa hedhi tofauti na zamani ambapo sasa zipo hadi taulo za kufua ambazo zinahitaji maji safi kwa ajili ya kusafisha baada ya kutumia hivyo ni wakati wa serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.
“Binafsi taulo za kufua zimenipunguzia gharama ya kununua kila mwezi nanunua mara moja kwa mwaka na kutumia kwa muda wa zaidi ya miezi 12, lakini changamoto ni maji hasa yanapokuwa ya mgao unashindwa kufua vizuri hali ambayo ni hatari kwa afya,”ameeleza Lydia.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi