November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTCL kusaidia kampuni zingine kufikisha mawasilino kwa wananchi

Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline ,Dodoma.

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga amesema shirika hilo linasaidia Kampuni zingine za simu kufikisha mawasiliano kwa wananchi kwa kuunganisha mkongo wa Taifa na kuingiza kipato kwa shirika na Serikali kwa ujumla.

Mha.Ulanga amesema kuwa hiyo ni kutokana na TTCL kuwa mtoa huduma ya mawasiliano kwa watoa huduma wengine kupitia mkongo wa Taifa.

Mkurugenzi huyo amesema hayo jijini hapa leo,Mei 13,2023 mara baada ya hafla ya utiaji saini mikataba ya kupeleka huduma za mawasiliano vijijini baina ya UCSAF na watoa huduma za mawasiliano ambapo minara 758 itajengwa na Shirika hilo linatarajia kujenga minara 54 kwenye Kata 104 na vijiji kati ya minara hiyo.

“Hapo awali mashirika mengine ya binafsi walikuwa wanasita sana kupeleka mawasiliano katika maeneo ya vijijini kwahiyo TTCL ilichukuwa fursa kuweza kupeleka mawasiliano vijijini na watoa huduma wengine waweze kufaidika na huduma za mawasiliano vijijini,”amesema.

Amesema wao kama shirika tayari wanazaidi ya maeneo 130 ambapo wao ndiyo watoa huduma pekee.

“Lakini hii inatuongezea maeneo mengine zaidi ya 104 ambapo sisi kama TTCL tutaweza kufikisha mawasiliano katika eneo kubwa la vijijini na tunamini tukiweza kukamilisha mradi huu wa mawasiliano sisi sote kwa ujumla tutaongeza zaidi usikivu wa mawasiliano katika maeneo ya vijijini hapa nchini kwetu na tutaweza kukuza uchumi wa kidigiti,”amesema.

Akizungumzia kuboresha huduma za mawasiliano nchini Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Shirika limeingia makubaliano na Shirika la Posta kwa ajili ya kutoa huduma za uwakala mkuu wa T-PESA, usambazaji wa vocha na usajili wa wateja wapya wa TTCL.

Amesema huduma za TTCL zinapatikana kila palipo na ofisi za Shirika la Posta na kuendelea kufanya maboresho ili
kuhakikisha huduma linazotoa zinakidhi viwango kwa kuboresha mitambo na kuongeza vituo vya huduma kwa wateja.