November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachimbaji wafikiwa kupitia clinic ya madini

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online Mwanza

WIZARA ya Madini na Taasisi zake zimeshiriki kuwasilisha mada mbalimbali katika Clinic ya Madini iliyoandaliwa na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) katika Maonesho ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza.

Maonesho hayo yalizinduliwa Mei 3, 2023 yanaenda sambamba na Wiki ya Madini pamoja na Kongamano la Mkutano Mkuu wa Kwanza wa FEMATA linalotarajiwa kufia kilele chake tarehe 09/05/2023.

Akitoa mada katika Clinic hiyo Mkurugenzi wa Kanzidata Terence Ngole amesema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imejipanga kikamilifu kuendelea kusogeza huduma za ugani kwa jamii ambapo mpaka sasa taasisi hiyo imefungua ofisi katika mikoa ya Kimadini ya Geita na Chunya na itaendelea kufungua ofisi katika mikoa mingine ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mtakwimu, Azihar Kashakara amesema Tume ya Madini inajukumu la kutoa leseni na kuzisimamia ambapo amewashauri wachimbaji wadogo wa madini kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Serikali hususan katika maeneo ya uchimbaji wa madini.

Naye, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Wanawake Tanzania (TAWOMA) Salma Ernest amesema Chama hicho kimeanda Tuzo ya Malkia wa Madini kwa lengo la kuwahamasisha wachimbaji wa Madini Wanawake kujiunga na chama ili wafaidike na rasilimali madini.

Pia, Salma ametoa wito kwa Wachimbaji wa Madini Wanawake nchini kujiunga na chama hicho ili kuwawezesha wanawake wengi zaidi kuinuka kiuchumi ambapo chama hicho kitawawezesha wanawake kuunganishwa na Taasisi za Fedha ili wapatiwe mikopo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji madini.

Wiki ya Madini inaenda sambamba na Maonesho ya Madini pamoja na Kongamano la Mkutano Mkuu wa Kwanza wa FEMATA ambao umebebwa na Kaulimbiu isemayo “Amani iliyopo Tanzania, itumike kuwa fursa kiuchumi na Tanzania kuwa kitovu cha Biashara ya Madini Afrika”.