Na Ikulu, Dar Es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewasili Jijini Dar es Salaam akitokea Makao Makuu Dodoma.
Akiwa Ubungo, Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma na kuelezea kufurahishwa kwake na kazi nzuri inayoendelea, pia amewasalimu wananchi wakiwemo viongozi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kando ya eneo la mradi huo.
Akizungumza kwa niaba viongozi wa vyama vya siasa na vijana wa Ubungo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Ubungo Ndg. Edwin Cyprian Mbena amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutekeleza vizuri na kwa vitendo Ilani ya CCM ikiwemo ujenzi wa barabara za juu katika eneo hilo, na ameeleza kuwa mradi huo umeleta heshima na unawanufaisha wananchi wa Ubungo na Jiji zima la Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mama mwenye Ulemavu wa miguu Nyangoma James mara baada ya kumchangia kiasi cha Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ununuzi wa Bajaji. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mama mwenye Ulemavu wa miguu Nyangoma James mara baada ya kumchangia kiasi cha Shilingi Milioni 5. kushoto aliyekaa ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makore Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mama mwenye Ulemavu wa miguu Nyangoma James kuhusu changamoto ya Usafiri wa Bajaji aliyokuwa akiomba kupewa ili imsaidie kuendesha familia yake
Amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaamini vijana na kuwapa nafasi za uongozi na amemuahidi kuwa vijana wamekubaliana kutomuangusha kwa kuhakikisha wanachapakazi na kusimamia maslahi mapana ya Taifa bila kubagua.
Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Ubungo kwa kupata mradi huo na ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 240 kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo na pia inajenga barabara ya njia nane (Kimara – Kibaha) kwa kuwa imedhamiria kuibadilisha Tanzania. Amewataka Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizo.
Baada ya kuwasalimu wananchi hao, Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia ununuzi wa pikipiki ya miguu mitatu kwa ajili Bi. Nyangoma James ambaye ni mwenye ulemavu, na amefanikiwa kukusanya shilingi 8,750,000/- zikiwemo shilingi 5,000,000/- alizotoa yeye mwenyewe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akicheza Wimbo wa hamasa pamoja na Wananchi wa Ubungo mara baada ya kuwahutubia. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiondoka katika eneo la Ubungo Darajani mara baada ya kuzungumza na Wananchi. PICHA NA IKULU
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili