Serikali yasaini mkataba wa bilioni 37.4.
Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online,Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesaini mkataba wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa na Mawasiliano katika wilaya 23 unaogharimu takribani Bilioni 37.4.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, amesema kuwa mradi huo unalenga kumaliza changamoto za mtandao katika wilaya hizo.
Amesema kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imepanga kutekeleza mradi wa kuimarisha mawasiliano katika ngazi ya Wilaya kwa kuunganisha Wilaya zote kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa mawasiliano ambayo yatachochea maendeleo katika Wilaya hizo, sambamba na wananchi kupata intaneti yenye kasi.
“Leo hii tunashuhudia utiaji wa saini mkataba wa upanuzi wa Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL
na Kampuni ya HUAWEI International kwa ajili ya ujenzi wa Kilometa
1,520 ambazo zitaunganisha kwenda katika Wilaya 23,”amesema.
Waziri Nape amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo utaondoa changamoto za mawasiliano katika Wilaya 23 ambazo zitaunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Amesema Wilaya hizo zinaenda kuwa na mawasiliano ya uhakika na yenye ubora ambayo yatasaidia katika shughuli za maendeleo na ujenzi wa taifa.
“Malengo yetu kama Wizara ni kuhakikisha unafikia lengo la kuunganisha Makao Makuu ya Mkoa na Wilaya ili kutoa fursa kwa serikali ya Mkoa na Wilaya kuimarisha mawasiliano ya ndani,pia kutoa fursa kwa taasisi umma na binafsi kufikisha huduma zao kwa wananchi kwa haraka,”amesema Waziri Nape.
Kadhalika amesema kuwa serikali kwa kutambua changamoto za Wilaya nchini kukosa mawasiliano ya uhakika ambayo yamesababisha wananchi katika Wilaya hizo kukosa fursa mbalimbali za kijamii na kibiashara hivyo imejipanga kuzitatua.
Ameeleza kuwa Mikoa yote nchi nzima imeishaunganishwa katika Mkongo wa Taifa ambao umefika katika vituo vya mipakani ambavyo vimepakana na nchi jirani, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi muhimu katika Ukanda wa
Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi TTCL Zuhura Muro ameshukuru serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuwezesha utekelezaji wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenda kwenye ngazi ya Wilaya.
Amesema ni siku muhimu kwa shirika hilo na taifa kwa ujumla kwa uwekezaji huo ambao unaenda kuimarisha sekta ya mawasiliano nchini na kuchangia katika kukua kwa sekta nyingine za maendeleo,
“Shirika la Mawasiliano Tanzania siku ya leo tunatia saini mkataba kati yetu TTCL na kampuni ya HUAWEI International, mkataba huu ni wa upanuzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano kwenda katika Wilaya 23 ikihusisha ujenzi wa Kilometa 1,520,”amesema.
Aidha amesema upanuzi huo wa mkongo wa taifa unakwenda sambamba na dira na malengo ya shirika katika kuhakikisha inakuwa mtoa huduma bora wa miundombinu ya mawasiliano data na simu kitaifa na kimataifa.
Huku akisisitiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi itashiriki kikamilifu katika kuhakikisha menejimenti inasimamia vyema mradi huo na miradi mingine inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Awali akitoa taarifa ya Shirika hilo Mkurugenzi Mkuu TTCL Mhandisi Peter Ulanga amesema mkataba huo ambao utasiniwa kati ya shirika hilo na HUAWEI International Co. Limited unatakiwa kukamilika ndani ya miezi 6 tangu kusainiwa kwa mkataba huo.
“Kukamilika kwa mradi huu utaondoa changamoto iliyokuwepo awali ya ukosefu wa mawasiliano katika wilaya 23 Kwa kuwa kuna wilaya zilikuwa hazina kabisa mawasiliano ya uhakika,” na kuongeza kuwa
“Nyingine zilitumia teknolojia ya microwave radio ambayo teknolojia hiyo ilikuwa na changamoto ya kuathiriwa na hali ya hewa sambamba na changamoto za uwezo mdogo hivyo kushindwa kutoa huduma ipasavyo,”.
More Stories
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake