Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema uwepo wa mashindano hayo ni fursa ya kipekee kuitangaza Tanzania Kimataifa na kuiletea manufaa kwa kufuatiliwa kupitia mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano.
Aliyasema hayo wakati akihutubia wananchi katika Mashindano makubwa ya Qur’aan ya Afrika mwaka 2023 yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam Aprili 9, 2023, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al Hikma Foundation, ambapo alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Hassan.
Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuongeza bidii kusoma Qur’aan mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani na hata baada ya mwezi kuisha ili kutekeleza ibada kwa usahihi.
Aidha, Dk. Mwinyi aliwahimiza watu wenye uwezo kutoa sadaka kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu kama yatima, wajane, walemavu, na wengineo hasa ndani ya mwezi huu wa Ramadhani.
Mashindano hayo makubwa ya Qur’aan ya Afrika mwaka 2023, ambayo yameshirikisha washiriki kutoka nchi ishirini za Afrika na washiriki watatu maalum kutoka Marekani, Uingereza na Saudia Arabia.
Pia, aliwakabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza kutoka Misri kiasi cha shilingi 23,900,000 na medali ya dhahabu na laptop moja.
Mshindi wa pili kutoka Senegal alipokea shilingi 15,300,000 na medali ya fedha.
Mshindi watatu kutoka Tanzania alipokea shilingi 10,280,000 na medali ya fedha.
Kwa upande wake, Sheikh Nurdin Kishki ambaye ni mwenyekiti wa taasisi ya Al-Hikma alisema Kupitia Taasisi yake vijana 50 watalipiwa mahari ambao wapo tayari kuoa na kusisitiza kuwa mahari hiyo haitawahusu wale wanaotaka kuongeza mke wa pili.
“Tutafanya ndoa ya pamoja ya watu 50 mahari tutatoa Sisi Al-Hikma Foundation masharti usiwe unaongeza mke wa pili ndoa itafanyika Dar es salaam chini ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir”
Alisema lengo lilikuwa kuozesha vijana 100 hivyo ametoa wito kwa yeyote mwenye kuweza kuunga mkono jambo hilo.
Aidha alisema jambo hilo litafanyika kupitia program maalum iliyoanzishwa na taasisi hiyo ya kurejesha kwa jamii kupitia mashindano hayo na kwa mwaka jana walifanikiwa kulipia gharama za kujifungua kwa wajawazito 100.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti